Habari za Punde

Mfumo Mpya wa Bajeti Umeonesha Mafanikio


Na Mwandishi wetu
KAMISHNA wa Bajeti Zanzibar, Khatib Mwadini Khatib, amesema mpango wa majaribio wa bajeti inayozingatia mipango maalum ya miradi ya utekelezaji (PBB), umeonesha mafanikio makubwa katika matumizi ya fedha za umma.

Kamishna huyo alieleza hayo jana hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyopo mjini hapa kwenye mkutano uliojadili mafanikio na changamoto za majaribio ya mpango huo wa bajeti.

Kamishna Khatib alisema majaribio hao yameonesha mafanikio mazuri wa utekelezaji wa bajeti za serikali kwa mipango iliyokusudiwa kwa mwaka wa bajeti wa 2011/2012.

Alisema majaribio yameonesha kuwa kila kipaumbele cha mradi wa bajeti kilichowekwa hutekelezeka na kupatiwa fedha zinazostahiki jambo ambalo linaweza kuipatia Zanzibar maendeleo ya kijamii kwa haraka.

“Malengo makubwa ya PBB, ni kuongoza na kuelekeza matumizi kwenye vipaumbele vilivyowekwa pamoja na kufanya matumizi sahihi”,alisema Kamishna huyo.

Alisema kuwa progamu hiyo imefanikiwa kwani mbali ya kupata fedha za kutekelezeka kwa miradi pia imekuwa ikiangalia sera na vipaumbele mahususi akitolea mfano suala la elimu ya juu.

Kamishna huyo alisema chini ya programu ya PBB, fedha zinazoingizwa huenda moja kwa moja kwenye mradi uliokusudiwa sambamba na kuangaliwa utekelezaji wake.

Katika mkutano huo Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na maofisa mbali mbali walishiriki kwenye mkutano huo.

Wizara za zilizo kwenye majaribio ya bajeti chini ya mpango wa PBB ni pamoja na wizara ya Afya, Kilimo na Maliasili, Elimu na Mafunzo ya Amali, Miundombinu na Mawasiliano, Ardhi Makaazi Maji na Nishati na wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha za Mipango ya Maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.