Habari za Punde

Milioni 10 Zaitesa ZFA . Yazisaka ili Kuendeshea Uchaguzi wa Rais


Salum Vuai, Maelezo
HUKU zikiwa zimebakia wiki tatu kabla kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kutafuta Rais mpya wa Cham cha Soka Zanzibar (ZFA), chama hicho kinahaha kusaka fedha kwa ajili ya kuendeshea uchaguzi huo.

Awali, ZFA ilitangaza kuwa inahitaji shilingi milioni kumi ili kugharamia shughuli zote za uchaguzi, ikiwa pamoja na nauli, gharama za malazi kwa wajumbe wa Kamati Tendaji kutoka Pemba pamoja na posho.

Tayari chama hicho kimeshatangaza Juni 30, mwaka huu kuwa ndio siku itakayofanyika uchazui huo kumsaka mrithi wa Rais wa zamani Ali Ferej Tamim ambaye aliamua kujiuzulu tangu Juni 2, kwa sababu za kiafya pamoja na kutingwa na shughuli za kifamilia.

Hata hivyo, hadi sasa chama hicho hakijapata fedha hizo, ingawa Msemaji wake Munir Zakaria, amesema wamepeleka ombi sehemu fulani, na wanasubiri kujua kama watapatiwa fedha hizo. au la.

Aidha sababu hiyo inaelezwa kuwa ndiyo inayokifanya chama hicho kishindwe kutangaza tarehe za kuchukua fomu, kurejesha na usaili kwa watu wanaotaka kuwania kiti hicho.

Zakaria alisema kama hawatafanikiwa kupata fedha huko wanakotegemea, watatafuta mkopo kutoka sehemu nyengine, na kuongeza kuwa hata yeye anaweza kukikopesha chama hicho, kwa nia ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kama ulivyopangwa.

"Tunasubiri baadhi ya wenzetu waliokwenda Kurdistan kwenye Kombe la Dunia, warudi na kikombe, ili tukae pamoja na kutangaza tarehe za kuchukua fomu, kurejesha na usaili kwa wagombea, na kuitaarifu Kamati ya Uchaguzi, ili hatimaye kukamilisha zoezi zima la uchaguzi wetu", alifafanua Zakaria.

Tayari wanamichezo kadhaa wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa Wazee SC Salum Bausi Nassor pamoja na mwandishi wa habari Masanja Mabula anayefanya kazi kisiwani Pemba, huku kukiwa na fununu zilizofichwa chini ya zulia, kwamba Mkurugenzi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View, naye anajiandaa kujitosa katika kinyang'anyiro hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.