Habari za Punde

Manji Ajitosa Uenyekiti Yanga

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ZOEZI la kuchukua fomu za kugombea uongozi wa nafasi mbalimbali katika klabu ya Yanga, likitarajiwa kufungwa leo saa kumi, mfadhili wa wakongwe hao Yussuf Manji, ni miongoni mwa wanaowania nafasi ya Mwenyekiti.

Wengine waliojitosa kwenye kugombea kiti hicho, ni Sarah Ramadhan, Edger Chibura na John Jambe.

Nafasi hiyo iko wazi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa akiishikilia Lloyd Nchunga.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti, wanaoikodolea macho nafasi hiyo ni Ayoub Nyenzi, Ali Mayay, Yono Kevela na Clement Sanga.

Taarifa hiyo pia imewataja wanaowania ujumbe wa Kamati Tendaji kuwa ni Aron Nyanda, Shaaban Katwila, Edger Fongo, Ramadhan Mzimba, Muzamil Katunzi, Lameck Nyambaya, Seif Ahmed, Abdallah Binkleb, Mohammed Mbaraka pamoja na Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliachim Masu.

Wengine ni Moses Katabaro, George Manyama, Omary Ndula, Abdul Mbaraka, Peter Haule, Justine, Abdala Sharia, Jamal Kisoingo, Yono Kevela na Gaudensius Ishengoma.

Mapema msanii nguli wa muziki wa taarab Mzee Yussuf ambaye alijitokeza kuwania ujumbe, alijiondoa sambamba na mchezaji wa zamani wa timu hiyo Ali Mayai Tembele.

Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Francis Kaswahili aliyetangaza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuchukua fomu jana.

Uchaguzi mkuu wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu, kufuatia wajumbe wengi wa Kamati ya Tendaji iliyoingia madarakani mwaka juzi, kujiuzulu akiwemo Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.