Habari za Punde

Mussa amuumiza kichwa kocha riadha


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


KOCHA wa Riadha wa timu ya Tanzania inayotarajiwa kushiriki mashindano ya Olimpiki London, Zakaria Gwandu, ameelezea kusikitishwa na kushangazwa kwa mchezaji Faustine Mussa kutojiunga na wenzake kambini, Mkuza Kibaha.
 

Mashindano hayo ya Olimpiki yanatarajiwa kufanyika jijini London, Uingereza kuanzia Julai 27 hadi Agosti 12 mwaka huu.


Kocha huyo amekaririwa jana akisema kuwao, wakati timu ikitarajiwa kuondoka nchini Julai 8 mwaka huu, Mussa ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi Tanzania, ndiye pekee ambaye hajajiunga na kambi hadi sasa, jambo alilosema linamuweka katika wakati mgumu kutekeleza programu zake.


“Ninachoweza kusema ni kwamba sifahamu kinachoendelea kuhusiana na mchezaji Faustine Mussa, sijui tatizo ni kwa mchezaji au mwajiriwa wake, kwani Chama cha Riadha kilikwishatuma barua ya kumuombea ruhusa mwajiri wake muda mrefu, lakini bado hajaonekana kambini,” alieleza kwa huzuni kocha huyo.


Timu ya riadha itakayoshiriki michezo ya Olimpiki nchini Uingereza, inaundwa na wachezaji wanne, ambao ni Zakia Mrisho, Samson Ramadhani, Msenduki Mohamed na Faustine Mussa, ambaye bado hajaripoti kambini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.