Habari za Punde

ZFA Isiingiliwe katika Utendaji Wake - Waziri

Na Salum Vuai, Maelezo

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, ametaka Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kisiingiliwe katika utendaji wake wala kubughudhiwa.


Akifungua mkutano wa uchaguzi mdogo wa Rais wa chama hicho kwenye hoteli ya Bwawani jana, Mbarouk alisema ni vyema ZFA iachiwe ifanye kazi zake za kuendesha soka kwa kufuata katiba na kanuni zake na kujipangia mikakati ya maendeleo kwa maslahi ya nchi.


"Natoa wito kwa taasisi zangu zote zilizomo ndani ya wizara yangu, kuiachia ZFA kufanya kazi zake kwa mujibu wa katiba na kanuni zake bila kuingiliwa", alisisitiza Waziri huyo.


Mbarouk alifahamisha kuwa, hata mashirikisho ya kimataifa ya mpira wa miguu kama vile FIFA, CAF na CECAFA, yanakataza vyama vyote vya soka kuingiliwa shughuli zao na serikali za nchi husika, isipokuwa katika masuala ya timu za taifa.


Alisema kwa hatua ambazo ZFA imezifikia katika siku za karibuni, ni dalili kuwa sasa inajiweza, na kuongeza kuwa wizara yake inakipongeza kwa dhati chama hicho.


Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupata mdhamini wa ligi kuu kwa kushirikiana na wizara, kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha Grand Malt, kumudu kuiandaa timu ya taifa Zanzibar Heroes na kuipeleka Kurdistan kwenye mashindano ya dunia kwa nchi ambazo si wanachama wa FIFA.


Aidha alisema kuandaa mashindano ya Kombe la Urafiki Tanzania yanayotarajiwa kuanza leo, ni ishara njema kwamba chama hicho kimeanza kukua na kuendesha mambo yake chenyewe.


Waziri huyo alielezea matumaini yake kuwa uchaguzi huo wa jana, utaleta faraja kwa Wazanzibari kwa kutoa mwanga na dira nzuri na njema  kwa maendeleo ya mpira wa miguu hapa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.