Na Husna Mohammed
TATIZO la umasikini uliokithiri umeelezwa
kuwa ndio chanzo kikubwa cha watoto Chini ya umri wa miaka 18 kujiingiza katika
ajira mbaya za watoto hapa Zanzibar.
Katika utafiti uliofanywa mwaka 2004/2005 na
ofisi ya Mtakwimu mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, umebaini kuwa nusu ya
watu wa Zanzibar ni masikini, jambo ambalo baadhi ya familia wamekuwa
wakiwategemea watoto wadogo katika kusaidia majukumu ya kifamilia.
Afisa wa Chama cha Waandishi wa Habari
wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA), Sheikha Haji Dau, alisema hayo wakati
alipokuwa akitoa mafunzo kwa wanawake wa Mkoa wa Kusini Unguja huko Dunga,
kuhusu mapambano juu ya ajira za watoto katika mkoa huo.
Alifahamisha kuwa Mkoa wa Kusini ni moja ya
mkoa wenye ajira nyingi za watoto hasa kutokana na mazingira ya bahari hivyo
watoto wengi wamekuwa wakijishughulisha na sekta ya uvuvi ambapo pamoja na
mambo mengine lakini familia zao zimekuwa zikiwategemea kutokana na kipato
kidogo wanachokipata.
Alifahamisha kuwa watoto wengi wamekuwa
wakifanyishwa kazi za hatari na kukoseshwa haki yao ya msingi ya elimu jambo
ambalo linamjengea mazingira mabaya kwa maisha yake ya baadae.
Alizitaja baadhi ya ajira mbaya kwa watoto
kuwa ni pamoja na kuwaingiza watoto katika biashara haramu ya madawa ya
kulevya, kufanyishwa kazi katika sekta ya kilimo, ufugaji, viwanda nakadhalika.
"Kuwatumia kuwakuwadia au kuwatoa kwa
ajili ya kufanya ukahaba na utengenezaji wa picha za ngono au katika maonesho
ya picha za ngono, uuzaji na usafirishaji haramu wa watoto, kuweka rehani kwa
ajili ya deni na kuwafanya vijakazi ni moja ya utumikishwaji wa watoto
ulioshamiri nchini," alisema Ofisa huyo.
Aidha alisema pamoja na mambo mengine lakini
Tanzania imekuwa ikiwatumikisha watoto kazi ya uyaya (majumbani) kutoka sehemu
moja kwenda nyengine jambo ambalo wakati mwengine linahatarisha ustawi wa
ukuaji wa watoto kutokana na kazi za ndani.
Sheikha alifahamisha kuwa watoto hao
wamekuewa wakipata madhara makubwa ikiwa ni pamoja na madhara ya kimwili,
kiakili na hata kimaadili.
Nao baadhi ya washiriki wa mkutano huo
kutoka katika vijiji vya Chwaka, Marumbi, Uzini na Charawe walikiri kuwepo kwa
watoto wanaotumikishwa katika familia zao ikiwa ni pamoja na kufanyishwa kazi
za uvuvi, kilimo, ufugaji na ukataji wa kuni jambo ambalo watoto wengi wanakosa
fursa ya kupata elimu ya lazima.
Mradi wa kuwatoa watoto katika ajira mbaya
umefadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU), ambao unasimamiwa na Mfuko wa kuwasaidia
watoto ulimwenguni Save the Children na watekelezaji wa mradi huo ni Chama cha
Waandishi wa Habari wanawake TAMWA Zanzibar wakishirikiana na Jumuiya ya
kuwaendeleza wanawake Zanzibar (COWPZ)
No comments:
Post a Comment