Habari za Punde

Idara Yagawa Vitambulisho Zaidi ya 10,578


Na Mwantanga Ame
JUMLA ya Wazanzibari 10,578 wamepatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi baada ya kukamilisha masharti ya kisheria ya kuweza kupata vitambulisho hivyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, aliyasema hayo jana wakati akisoma hotuba ya  bajeti ya Mapato na Matumizi ya Ofisi kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Waziri Mwinyihaji, alisema ndani ya kipindi cha mwaka huu wa fedha Wazanzibari 10.578 wamefanyiwa usajili kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.


Alisema katika usajili huo jumla ya vitambulisho vipya 3,923 vilitengenezwa baada viliopo kumaliza muda wake wa matumizi huku wafanyakazi wa serikali waliopatiwa huduma hiyo walifikia 10,393.

Alisema hivi sasa Idara hiyo pia imeshaandaa rasimu kwa ajili ya kuifanyia marekebisho sheria namba 7 ya 2005 ikiwa ni hatua ya kutoa vitambulisho kwa wageni wanaoishi hapa nchini.

Alisema rasimu hiyo tayari imeshapitishwa na Baraza la Mapinduzi na hivi sasa inasubiri kufikishwa katika Baraza la Wawakilishi ili kuweza kuanza kujadiliwa.

Alisema tangu mfumo huo kuanza kutumika Idara hiyo imeweza kuhakikisha inatimiza masharti ya kimataifa kwa mara ya sita mfululizo na imeweza kushinda kufikia viwango bora duniani.

Alisema kwa ujao wa fedha itaendelea kusajili Wazanzibari 10,500 wanaotimiza masharti ya usajili na kuwapatia vitambulisho pamoja kutengeza vitambulisho kwa waliomaliza muda.

Akizungumzia juu ya Idara ya Usalama Kazini (GSO), Waziri huyo alisema jumla ya wafanyakazi 554 kutoka katika taasisi mbali mbali za serikali walifanyiwa upekuzi na taasisi 12 zilikaguliwa kuangalia utunzaji wa siri za seriakali.

Akizungumzia Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa shughuli za Wazanzibari Wanaoishi Nchi Nje, alisema kimeweza kufanya ziara mbali mabali katika nchi za falme za kiarabu kwa Oman na Dubai ikiwa ni hatua kukutana na Wazanzibari ili kuwashajiisha katika kushiriki kuchangia maendeleo ya Zanzibar

Akizungumzia juu ya mradi wa mageuzi ya Serikali za Mitaa Waziri huyo alisema sera yake imekamilika baada kupitishwa kwa wadau tofauti zikiwemo taasisi binafsi ikiwa ni hatua ya kupata maoni yao.

Aidha, upande wa uratibu wa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Waziri huyo, alisema tayari kuna mradi ambao utahusisha ujenzi wa misingi ya maji ya mvua kwa ajili ya maandalizi ya kutafuta mkandarasi ataeifanya kazi hiyo ambayo inatarajiwa kuyanufaisha maeneo ya ziwa la Sebleni, Ziwa la Mtumwajeni na Ziwa la kwa binti Amrani.

Maziwa mengine yatayofaidika na mradi huo Waziri huyo alisema ni la Mantenga, Kwamtipura, Kilima hewa karakana, Sogea, Mpendae, Jang’ombe, Uwanja wa Demokrasia na Shauri Moyo.

Akizungumzia juu ya shughuli za Mikoa yote ya Unguja na Pemba Waziri huyo alisema walifanikiwa kwa kiai kikubwa kutekeleza bajeti zao huku wakisimamia utekelezaji wa utoaji wa huduma za kijamii kwa kushirikia katiika kampeni mbali mbali za chanjo kwa watoto pamoja na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama, kusimamia mapato pamoja na kutoa mchango wa kupambana na maradhi ya ukimwi.

Akizungumzia juu ya shughuli za Idara Maalum za SMZ, alisema nazo zimeweza kutekeleza vyema majukumu yao ya kiulinzi na kutoa huduma mbali mbali katika jamii.

Akifafanua waziri huyo alisema katika Idara ya Mafunzo serikali iliweza kuwahudumia wanafunzi 479 ambapo kati ya hao 17 ni wanawake ikiwa ni ongezeko wanafunzi 17 waliopokelewa kwa mwaka 2010/2011 huku mahabusu wakifia 2,620 ambapo kati ya hao 2,510 wanaume na wanawake ni 110 ambapo makosa yao makubwa ni wizi kutumia nguvu, kubaka, kunja nyumba na kuiba wizi wa mazao na shambulio.

Upande wa Idara ya Zimamoto Waziri huyo alisema, nayo imeweza kufanya kazi vizuri ikiwa pamoja na kupata kifaa kipya cha kuzimia moto cha Dry Sprinkler Power Aerosal (DSPA).

Idara ya Valantia, Waziri huyo alisema kimeweza kuisaidia serikali katika kusimamia vyema kazi za uchumaji wa karafuu katika msimu uliomalizika.

Kuhusu Kikosi cha JKU, Waziri huyo alisema, kimefanya mapitio ya uendeshaji wa shamba la Bambi la mboga mboga ili liweze kuwa na tija iliyokusudiwa.

Akizungumzia juu ya kikosi cha KMKM, alisema serikali kwa mwaka uliopo wameweza kukipatia vifaa kiasi cha kuweza kukamata mafuta ya dizeli lita 25,950  petro ;o lita 1,790 sukari kilo 20,250, mchele kilo 76,800 na karafuu mbichi 200

Waziri huyo aliwaomba Wajumbe wa baraza hilo kumuidhinishia shilingi 50,698.1 milioni kati ya hizo shilingi 46,654.1 milioni kwa matumizi ya Kawaida na kazi za maendeleo ni shilingi 1,906.0 milioni na shilingi 2,138 milioni ni ruzuku kwa Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.