Ataka isichonganishwe na mataifa ya nje .
Na Ramadhan Makame
WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Massoud Hamad amesema kuwa Zanzibar haifungiki na inayo mamlaka kwa mujibu wa sheria za ndani za kimataifa kusajili meli za kigeni kutoka nchi yeyote duniani.
Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi
wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akitoa taarifa ya serikali kwa wajumbe wa
Baraza hilo, kuelezea kuwa hakuna meli zilizosajiliwa Zanzibar zenye kufanya
biashara ya mfuta nchini Iran.
Serikali imelazimika kupeleka taarifa katika
Baraza la Wawakilishi kufuatia katika kikao cha juzi Mwakilishi wa jimbo la Mji
Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu, kutaka kujadiliwa kwa hoja hiyo kwa dharura.
“Kulingana
na “United Nations Convention Law of the Sea”, Article 91, na za “Geneva
convection of Registration” articles 6, 7 na 8, na kulingana na Zanzibar
Maritime Transport Act of 2006, section 8, Zanzibar ikiwa ni nchi moja kati ya
nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayo haki ya kusajili
meli yoyote kulingana na taratibu na sheria za Zanzibar, na sheria za kimataifa
zinazoongoza usajili huo”, ilieleza taarifa hiyo.
Alisema pamoja na Zanzibar kuwa na uwezo
kisheria wa kusajili meli, imekuwa ikifanya kazi hiyo kwa umakini na hakuna
meli za Iran zilizosajili zenye kupeperusha bendera za Tanzania kwa kukwepa
vikwazo.
Alifahamisha kuwa vyombo vya habari
vilivyoandika taarifa hizo vilikuwa na malengo ya uchonganishi na kwamba hakuna
meli hata moja ya Iran iliyosajiliwa katika Mamlaka ya Usafiri wa Bahari.
Waziri Hamad alisema katika suala lisilo la
Muungano kama la usafiri wa bahari, Zanzibar isiingiliwe katika utendaji wake
kama vile ilivyokuwa haiingilii SUMATRA, ila inaweza kupokea ushauri.
Waziri huyo alifafanua kuwa katika muda wa
wiki mbili kampuni zilizosajiliwa Zanzibar hakuna hata moja inayotoka nchini
Iran ambapo zote zinatoka katika nchi za Cyprus na Malta.
“Hii ni biashara
yenye kuipatia mapato makubwa serikali, kusajili meli 11 zaenye jumla ya GRT
1,388,368 tons, hivyo suala lisiwe sababu ya kuleta uchonganishi na kuharibu
mahusiano ya Zanzibar na nchi za nje, Zanzibar isishirikishe na mambo
hayo”,alisema waziri huyo.
Alieleza
kuwa Zanzibar ina uhusiano mkubwa na wa muda mrefu na nchi nyingi ikiwemo Iran
na hivi karibuni ilipata ugeni wa Makamo wa Rais wa Iran na viongozi wa nchi
hiyo walifanya mazungumzo namna Iran
itakavyoendelea kuisaidia Zanzibar katika miradi ya Maendeleo.
“Zanzibar
haingependa kuingizwa kwa visingizio vyovyote na kwa njama zozote katika
migogoro isiyowahusu”,alisema waziri huyo.
Akizungumzia
juu ya meli nyingi za kimataifa zinazosajiliwa Zanzibar kuwa zimechakaa,
alisema kabla ya meli hizo kusajiliwa hukaguliwa na wangalizi kimataifa na
kijiridhisha kuwa zinaubora wa kufanya kazi.
No comments:
Post a Comment