Na
Mwantanga Ame
KODI
za mishahara ya wafanyakazi wa Utumishi wa umma wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, wanaofanya kazi zao Zanzibar, itaingizwa katika mfuko
mkuu wa Hazina wa Serikali ya Zanzibar.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
kukubaliana katika vikao vya kutatua kero za Muungano vilivyopita ya kutaka
fedha za kodi za watumishi wa Serikali ya muungano waliopo Zanzibar kubakia
Zanzibar.
Wafanyakazi
hao ni pamoja na Taasisi za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Simu Tanzania (TCCL), Shirika la
Posta Tanzania, Benki Kuu Tanzania (BOT) na Taasisi za kibenki zilizofungua
matawi Zanzibar ikiwemo NMB, CRDB, Exim Bank na KBC.
Taasisi
nyengine ambazo zitaingia katika mkumbo huo ni pamoja na Idara ya Mambo ya Nje,
Idara ya Muungano, Ofisi ya Bunge, Makampuni ya simu pamoja na taasisi binafsi
ambazo zimefungua matawi yake Zanzibar baada ya kusajiliwa Tanzania Bara
yakiwemo Mashirika ya Bima.
Serikali
itachukua hatua hiyo kutokana na mfumo uliopo hivi sasa kodi hizo zimekuwa
zikiingia katika mfuko Mkuu wa Hazina wa Tanzania bara jambo ambalo limeonekana
haliko sahihi utekelezaji wake.
Hapo
awali, Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Omar Yussuf
Mzee, akielezea suala hilo alisema tayari limeshamaliza mjadala wake na hivi
sasa limo katika vikao vya watendaji kwa ajili ya kufanyiwa mabadiliko ya
sheria ya fedha ya Serikali ya Muungano ili kuwezesha fedha hizo kuingia
Zanzibar.
Akijibu
masuala ya waandishi wa habari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema tayari Serikali ya Muungano imeshatayarisha
sheria hiyo na inatarajiwa kupelekwa bungeni kwa hatua za kisheria.
Alisema
kuja kwa fedha hizo ni sehemu ya muendelezo wa kutatua kero za Muungano ambapo
tayari mambo kadhaa yameshafanyika na hivi sasa baadhi yake yanasubiri
mabadiliko ya kisheria.
Akitaja
mambo hayo alisema ni pamoja na suala la mafuta na gesi asilia baada ya
serikali ya Zanzibar kutaka kutolewa katika mambo ya Muungano ambapo sasa lipo
katika hatua za kisheria na Kamati ya Fedha ya Pamoja (JFC).
Sambamba
na hilo, masuala mengine ni Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu vipi Zanzibar
inaingia ambapo mjadala wake unaendelea katika upande wa kisiasa, Uvuvi wa
Bahari Kuu ambao Zanzibar imeamuliwa kuwa ndio Makao Makuu ambapo linasubiri kutatuliwa
kisheria.
Mambo
mengine aliyoyataja Dk. Shein ni suala la ajira kwa wazanzibari kwenye taasisi
za muungano, ushirikiano wa taasisi za Nje katika mambo ya mikopo, Bodi na
Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Usajili wa vyombo
vya moto kutoka Zanzibar ambao umefikia katika hatua nzuri, ongezeko la bei ya
umeme kwa Zanzibar kutoka TANESCO, uharamia, mfuko wa maendeleo ya Jimbo.
No comments:
Post a Comment