Na
Haji Nassor, Pemba
JUMLA
ya familia 11 zenye wakaazi zaidi ya 70 huko Shehia ya Kangagani Wilaya ya Wete
Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamelazimika kuzihama nyumba zao baada ya kukumbwa na
upepo mkali na kuezua mapaa na kupasuka kwa kuta.
Upepo
huo uliotokea jana wakati waumini wa dini ya kiislamu wakiendelea na sala ya
Ijumaa, ambapo ulisababisha kuwahamisha wakaazi hao kutokana na dhoruba hiyo iliyowapa
hofu kubwa juu ya usalama wao.
Akizungumza
na Gazeti hili kwa njia ya simu, Sheha wa shehia hiyo Fakih Omar Yussuf alisema
wakati wakiendelea na sala, ndipo upepo huo ambao alidai uliodumu kwa dakika 10,
ulipovuma na wao baada ya sala kukimbilia eneo hilo.
Alisema
walipofika eneo ambalo nyumba hizo 11 zilikumbwa na zahma hiyo, waliona mapaa
ya nyumba yakiwa yako mbali na nyumba na
baadhi ya kuta za nyumba za tofali zimepasuka vibaya.
‘’Kwa
kweli tulipofika wengi hatukuamini kwamba hasara hiyo imesbabishwa na
upepo,maana kuta za nyumba tena za tofali zimeharibika vibaya mno, na mapaa
yako mbali sana na nyumba zenyewe’’,alieleza kwa masikitiko Sheha huyo.
Akizitaja
familia hizo alisema ni pamoja na nyumba ya Khamis Ali Shehe, Juma Faki Hassan,
Fatma Juma Salehe, Haji Fakih Kombo, Mgeni Amour Shaame, Shaali Muhidin Juma, Saleh Ali Hassan na Said
Juma Bakar.
Sheha
huyo alisema kwa sasa taratibu zinazoendelea, ni kuwatafuta Polisi pamoja na
kitengo cha maafa ili wafanye taratibu nyengine za kuwasaidia waathirika hao
ili wapate makaazi ya kujihifadhi wakati huu wakiwa wamekumbwa na kadhia hiyo.
Alisema
kuwa kwa sasa baadhi ya wananchi waliokaribu na waaathirika hao wamekuwa
wakiwasaidia wenzao waliopata athari hiyo, kwa kuwakusanyia vitu vyao karibu na
makaazi yao ikiwa ni pamoja na bati na vitu vya matumizi ya ndani.
Alisema
hili ni tukio la mwanzo kuwahi kutokezea katika kijiji chao katika siku za hivi
karibuni na hadi anazungumza na mwandishi wa habari hizi hasara kamili
haijambulika.
No comments:
Post a Comment