Habari za Punde

Tani 245 Mchele Mbovu Zarejeshwa Pakistan


Na Fatma Kassim, Maelezo

BODI ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar imerejesha ilikotoka Pakistani mchele tani 245 aina ya Alminara, baada ya kubainika kuwa haufai kwa matumizi ya mwanadamu.

Mchele huo ulioingizwa nchini mapema mwezi uliopita, ulikuwa tani 260 ambapo baada kuruhusiwa kwa makontena saba na wafanykazi wasiowaaminifu wa Bodi hiyo waliopo Bandarini na ulisababisha kufika masokoni na kusababisha kupungua kwa tani 14.

Mkaguzi wa Chakula wa Bodi hiyo, Khamis Ali Omar, alisema zoezi zima la kukusanya mchele huo umefanywa na Bodi hiyo na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mwenye mali hiyo lilifanyika mara baada ya kuonekana mchele huo haufai kwa matumizi ya mwanadamu.


Alifahamisha kuwa hivi sasa Bodi inafanya kila jitihada ya kuusaka mchele huo katika maduka na wakifanikiwa kuuona watahakikisha unaangamizwa ili usiweze kuathiri watumiaji wa mchele huo.

Amewataka wananchi wakiuona mchele huo ama bidhaa yoyote ambayo wataitilia shaka kutoa taarifa kwa bodi hiyo ili kuweze kuchukuliwa hatua zinazofaa ikiwemo kufanyika kwa uchunguzi ili zisiweze kuleta athari kwa wananchi.

Kwa upande wa mfanyabiashara huyo Mohammed Mauliy ameishukuru Serikali kwa kuweza kumpatia kibali ambacho kitamuwezesha kurejeshewa gharama zamchele wake huo.

Aidha ameilaumu kampuni MSC iliyomsafirishia mchele huo kutoka Pakistani kwa kumsababishia hasara kubwa ikiwa ni pamoja na mpaka sasa kutumia karibu milioni 60 kwa usafirishaji tu na kuwataka wafanyabiashara wengine wasitumie kampuni hiyo.

Alifahamisha kuwa kutokana na gharama kubwa zitokazotumika kwa kusafirishia hapa Zanzibar watausafirisha mchele huo hadi Mombasa kwa tajiri mwenyewe na baadae kufanya utaratibu wa kuusafirisha kuelekea Pakistan.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.