Na Mwantanga Ame
KUNDI la wananchi lilifurika katika Idara ya Vizazi na Vifo wakiwa na malalamiko ya kuchelewa kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wao huku miezi kadhaa ikipita.
Wananchi hao waliokuwa na hasira walisema wamechoka nenda rudi ya kila siku na pale wanapofika ofisini hapo hakuna vyeti wanavyopewa huku ikizingatiwa kuwa tayari wameshalipia huduma hiyo.
Wakizungumza na Zanzibar Leo, baadhi ya wananchi hao akiwemo Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Matemwe, Juma Mcha alisema wamechoshwa na hali kwani Idara imekuwa ikiwapa usumbufu wa kuvufuata vyeti hivyo bila ya mafanikio.
Alisema amekuwa akilipia nauli ya zaidi ya shilingi 2,000 kwa kila safari aifanyayo kwa ajili ya kufuatilia cheti cha mtoto wake mjini, ambapo akifika hupigwa danadana bila ya kupatiwa cheti hicho kwa kutakiwa aje siku nyengine.
Alisema mbali ya kupoteza nauli kukifuata cheti hicho, pia amekuwa kipoteza muda wa kazi kwa kuvifuata vyeti hivyo, ambapo kila akifika huambiwa havijakamilika.
“Kama wanataka rushwa watuambie sio kutusumbua kama hivi, kuna watu utasikia amezaa juzi cheti ameshapewa baada ya wiki mbili tuu, sasa sisi tunokaa vijijini huku tunasumbuliwa waseme tuu tuwape rushwa”, alisema.
Alisema kazi ya kufuatilia vyeti hivyo vinavyowahusu wanafunzi wake 14 aliianza mwezi Machi mwaka jana lakini mwanzoni mwa mwaka huu alitakiwa kurudi tena mwezi wa Aprili lakini alipoenda aliambiwa kufuata tarehe ya jana.
Alifahamisha kuwa hawaelewi ni kwanini wanafanyiwa vituko hivyo wakati wakiwa tayari wameshalipa malipo yote waliotakiwa kufanya ili kupata vyeti hivyo.
Kutokana na hali hiyo kundi la watu waliokosa vyeti hivyo waliamua kuuzonga mlango wa ofisi hiyo baada ya kuzuiliwa na mmoja wa ofisa wa taasisi hiyo kuingia ndani huku akiwaita watu wengine kwa kumpitisha mmoja baada mwengine huku wengine wakitoa maneno kuishutumu taasisi hiyo.
Hasira za watu hao zilisababisha kuwageukia vyombo vya habari kwa kukataa kuelezea maoni yao kwa kudai hata wakisema hakuna wa kuwasikiliza kwani wamechoka na usumbufu wanaopewa na taasisi hiyo.
Kutokana na hali hiyo waziri Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari alilazimika kufanya ziara ya ghafla ambapo alikuta masongamano mkubwa wa wananchi anaohitaji kupatiwa vyeti hiyo.
Mapema mmoja wa ofisa aliepewa kuzuiya watu hao wa taaasisi hiyo kukataa kata kata kuruhusu Waandishi wa Habari, kwenda kumuona Mrajisi wa Vizazi na Vifo kwa kudai hakuwapo nchini huku akieleza kuwa kwa wakati huo hawaruhusu watu kwa vile Waziri anafanya ziara ndani ya ofisi hiyo.
Uchunguzi wa Zanzibar Leo kutoka ndani ya ofisi hiyo, umebaini tatizo hilo limesababishwa na kutowekewa saini vyeti hivyo na Mrajis kwa vile tayari vipo mezani kwake.
Mmoja ya chanzo cha habari hii ambaye hakutaka kutajwa jina alisema katika ofisi ya Mrajis, ameshafikishiwa vyeti vipatavyo 60 lakini bado hadi sasa havijawekewa saini na hawajui ni kutokana na sababu gani.
Assalaam alaykum
ReplyDeleteWadau kusema kweli sijui haya matatizo ya kufanya kazi kwa kujisikia yataendelea mpaka lini katika baadhi ya ofisi za serikali? Iweje Mrajisi ashindwe kutia saini katika vyeti ambavyo havimchukulii hata nusu saa kumaliza kazi hiyo? Hik tabia ya kuhangaisha wananchi kupataa huduma ambazo wameshaazilipia inavunja moyo! Kama mtu hawezi dhamana aliyopewa kwa nini akaikubali? Nashauri wafanyakazi wenzangu tuwajibike kwa ajili ya Taifa letu. Cheo ni dhamana na haya mambo hayaishii hapa duniani, hata mbele ya Mungu tutakwenda ulizwa. Ni bora kama mtu ameshindwa kufanya kazi aachiye ngazi na wengine wapewe nafasi. Nilipata kwenda pale kudai cheti cha jamaa yangu, basi nikaambiwa na afisa mmoja hebu lete elfu mbili nikampe bosi aweke sign upate cheti chako. Sasa inaonekana hiyo ndio tabia ingawa wananchi hawaambiwi ukweli. Tumechoshwa na tabia hizi chafu, ni wakati wa kubadilika sasa.
Wacheni kusumbua watu, kazi hii ilikuwa aifanye Sheha tu ofisini kwao, baadae wao masheha ni kuwasilisha reporti makao makuu
ReplyDelete