Habari za Punde

Zanzibar Itaendelea Kushirikiana na Sweden Kukuza Uhusiano


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi wa Sweeden nchini Tanzania bwana Jennerth Hjelmaker, alipofika Ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana mawazo. Kushoto ni mshauri wa balozi huyo bibi Margareta Brisman.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweeden nchini Tanzania bwana Jennerth Hjelmaker, huko ofisini kwake Migombani. Kulia ni mshauri wa balozi huyo bibi Margareta Brisman. (Picha zote na, Salmin Said, OMKR)

Na Hassan Hamad OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana na Sweeden katika kukuza uhusiano wake ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imekuwa mshirika wa karibu wa maendeleo kwa Zanzibar.

Maalim Seif ameeleza hayo huko ofisini kwake Migombani alipokuwa na mazungumzo na balozi wa Sheeden nchini Tanzania bwana Jennerth Hjelmaker.



Amesema Zanzibar inathamini sana mchango unaotolewa na nchi hiyo hasa katika sekta za elimu na afya, na kwamba itaendelea kushirikiana na nchi hiyo katika sekta mbali mbali kwa maslahi ya pande hizo mbili.

Makamu wa Kwanza wa Rais amefahamisha kuwa Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika sekta ya elimu na kupelekea kuvuka malengo ya uandikishaji wa wanafunzi wenye sifa ya kuanza kwenda skuli.

Hata hivyo Maalim Seif amesema licha ya mafanikio hayo, bado Zanzibar inakabiliwa na tatizo la upungufu wa walimu wa Sayansi pamoja na vikalio katika skuli mbali mbali Unguja na Pemba.

“Tumepata mafanikio mazuri katika sekta hii lakini bado tuna upungufu wa walimu wa sayansi pamoja na vikalio. Hii ni kutokana na kuwa vijana wengi wanasoma masomo ya sanaa na kutojishughulisha na masomo ya sayansi pamoja na yale ya lugha za kigeni”, alibainisha Maalim Seif.

Amesema kwa sasa serikali imeweka mkakati wa kuwashajiisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya masomo hayo, ili kuweza kupunguza au kuondosha kabisa tatizo hili katika siku zijazo.

Kwa upande mwengine Maalim Seif amesema ipo haja kwa nchi hizo mbili kukaa pamoja ili kutathmini mchango unaotolewa na Sweeden kwa Tanzania, na kuhakikisha kuwa unawafikia walengwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Nae balozi wa Sweeden nchini Tanzania bwana Jennerth Hjelmaker amesema nchi yake inafurahia uhusiano mwema uliopo kati yake na Tanzania na kutaka uendelezwe zaidi kwa maslahi ya nchi hizo mbili.

Balozi Jennerth amefahamisha kuwa Sweden ambayo imekuwa ikishiriana kwa karibu na Tanzania hasa katika masuala ya watoto na haki za binadamu kwa ujumla, itaendelea kutoa ushirikiano wake katika maeneo tofauti, ili kuendeleza uhusiano huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.