Habari za Punde

Zitto Ataka Bajeti Iondolewe Bungeni

DODOMA

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini ambaye ni waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Zubeir Kabwe, ameitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano kuiondosha Bungeni bajeti iliyoiwasilisha wiki iliyopita.

Zitto kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alieleza hayo jana Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani juu ya Bajeti mpya ya mwaka 2012/2013.

Alisema bajeti hiyo inapaswa kuondoshwa na kutayarishwa mpya ambayo itakidhi matakwa ya mpango wa maendeleo kama ulivyoainishwa na Bunge na kusainiwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

“Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iiondoe (withdraw) Bungeni bajeti iliyoileta ili ikatayarishwe upya ili ikidhi matakwa (compliance) ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na kusainiwa na Rais wa nchi”, alisema Zitto.

Aidha waziri huyo kivuli hakukubaliana na mpango wa serikali uliopo kwenye bajeti hiyo ambapo suala la kugharamia maendeleo limetengewa bajeti ya asilimia sufuri ya mapato ya ndani.

Alilifahamisha Bunge hilo kuwa kitendawili cha kuwa na uchumi unaokua kasi lakini haupunguzi umasikini kinaweza kikateguka kwa kuelekeza nguvu vijijini waliko Watazania wengi.

Alisema ni robo tatu ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo hawajui hadithi kukua kwa uchumi zinazoimbwa na kupewa sifa kila siku, na kueleaza kuwa wananchi hao wamekuwa na changamoto kadhaa zikiwemo maji, umeme, mazao kutofika sokoni, hawana barabara nzuri na skuli.

Akizungumzia juu ya fedha za rada shilingi bilioni 72.3, Zitto alisema kambi ya upinzani inahitaji maelezo kutoka serikalini juu ya utaratibu uliotumika kwa matumizi ya fedha hizo bila ya kupitishwa na Bunge.

“Mheshimiwa Spika, wakati Kamati za Bunge zilipokaa kujadili taarifa ya serikali kuhusu mfumo wa mapato na matumizi, waziri wa Fedha na Uchumi alitoa taarifa kuhusu fedha za rada zilizorejeshwa, jumla ya shilingi 72.3 bilioni ambazo zilipokelewa Machi 26, mwaka 2012, kwa mshtuko wa wabunge, waziri aliiambia kamati kuwa mchakato wa manunuzi ya vitabu na madawati kwa kutumia fedha hizi ulikuwa umeanza, fedha hizi hazijawahi kupitishwa na Bunge lako tukufu”.alisema Zitto.

Alisema kitendo cha serikali kuzitumia kabla ya kupitishwa na Bunge ni kuvunja sheria za fedha kuhusiana na masuala ya bajeti, ambapo waziri akizwasilisha hotuba yake hakugusia suala la fedha zilizorejeshwa kutokana na ununuzi wa rada.

Zitto pamoja na kumpongeza waziri William Mgimwa na Manaibu wake Saada Mkuya na Janeth Mbene kwa kupata nafasi hizo aliwatahadharisha kuwa wizara hiyo sio lele mama.

“Ninawapa pole maana wizara ya Fedha sio wizara lelemama. Kambi ya upinzani itaendelea kuisimamia wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha”,alisema Zitto.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.