Habari za Punde

Membe Aitolea Ufafanuzi Taarifa ya APRM

Na Kunze Mswanyama, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema taarifa ya APRM iliyokuwa isomwe na Rais Jakaya Kikwete haijashindikana kutokana na Tanzania kudaiwa dola 800,000.

Waziri huyo alieleza hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa taarifa hiyo itasomwa mjini Lilongwe nchini Malawi ifikapo Januari mwakani.

Membe alisema baadhi ya vyombo vya habari vilivyoandika kuwa Rais Kikwete ameshindwa kuisoma taarifa ya APRM Tanzania kwa wakuu wa nchi za Afrika kutokana na deni sio za kweli na walilenga kuupotosha kwa umma.

“Nikiwa safarini nilipata habari kuwa taarifa ya Tanzania huenda isisomwe kutokana na kudaiwa fedha, taarifa hizo ni potofu na wananchi nawaomba waelewe kuwa taarifa haitasomwa kutokana na kuwepo kwa mchakato mrefu siyo deni”,alisema waziri Membe.

Alisema hata Tanzania ikidaiwa mamilioni deni halitaathiri kusomwa kwa taarifa ya ndani ya kujitathmini kiutawala bora kwa wakuu wa nchi za Afrika.

Alifahamisha kuwa APRM ilikwishazunguka nchi nzima hivyo wameandaa masuali ambayo yanatakiwa kuja kujibiwa hapa nchini, hivyo siyo kazi ya siku moja ni jambo la muda mrefu na hatujapata taarifa lini watakuja nchini kuleta maswali hayo.

Mpango huo unaoratibiwa na Umoja wa Afrika, ulibuniwa ili kuweka hali ya utawala bora kwa nchi za kiafrika ambapo kila nchi inayotaka kuwa mwananchama ni lazima APRM wajiridhishe hasa baada ya kupewa vigezo ambavyo inatakiwa kuvikamilisha kabla ya kuwa mwananchama.

Akitoa ufafanuzi juu ya madai ya kuibiwa kwa fedha za safari za Rais,a alisema fedha hizo zilirudishwa benki na kuahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo unaohusisha taratibu za utoaji fedha zilizofanywa na viongozi waliokuwa wakikaimu nafasi hizo.

“Naomba nieleze kuwa, hadi sasa hakuna mtu yeyote tuliyemshaka kuiba, uchunguzi wa awali umebainisha kuwa hakuna senti hata moja iliyoibwa bali tutachunguza kwa makini kama taratibu za uhamishaji fedha zilifuatwa naomba wananchi waelelewe hivyo”,alisema.

Alisema tume imeundwa kuchunguza kupotea kwa zaidi ya shilingi bilioni 3.5 ambayo inashirikisha usalama wa Taifa, Mkaguzi Mkuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na idara ya ukaguzi wa ndani wizarani hapo.

Katika hatua nyengine waziri huyo alitumia fursa hiyo kukanusha taarifa kuwa amekitabiria ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.