Sera kujifungua bure kutekelezwa
Tani za vyakula vibovu zaangamizwa
Na Ramadhan Makame
WAZIRI wa Afya, Juma Duni Haji, amesema sekta ya afya pamoja na kupata
mafanikio, lakini inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo tatizo sugu
la upungufu wa wataalamu.
Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
alipokua akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha
2012/2013 mbele ya wajumbe wa Baraza hilo.
Alisema tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikibwa na gharama kubwa za
kuwafundisha wataalamu wa afya ambapo kwa miaka mitano mtaalamu mmoja
hutumia kiasi cha shilingi milioni 70.
Aidha alisema changamoto nyengine inayowakabili wataalamu hadi
kusababisha kuondoka nchini ni uduni wa maslahi pamoja na
kutozingatiwa malipo yao muhimu.
Aidha waziri huyo alisema serikali itabeba mzigo wote wa gharama kwa
akina mama wajawazito wakati wa kujifungua kwa hospitali zote.
“Kwa niaba ya serikali napenda kurudia tena kujifungua sasa ni bila ya
malipo kwenye hospitali za serikali”, Waziri Duni aliwaeleza wajumbe
hao kwa msisitizo.
Aidha waziri huyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa
sahihi bila ya woga pale watakapokabiliwa na changamo isiyopendeza
kutoka kwa watendaji.
Waziri huyo alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kutoa tamko kubwa na zito la
kufutwa kwa ada za wajawazito wakati wa kujifungua, tamko ambalo
lililenga kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Akizungumzia juu ya tatizo la vyakula vibovu vinavyoingizwa nchini,
alisema Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi kwa mwaka mmoja uliopita,
imezuia kuingizwa nchini jumla ya tani 780 na kuteketeza tani 5.48 za
vyakula visivyofaa kwa wanadamu.
Waziri huyo alisema tani 780 zilizozuiliwa kuingia nchini zilikuwa za
unga wa ngano ambao baada ya uchunguzi ulibainika kuwa haufai kwa
matumizi ya wanadamu.
Alisema katika mwaka huo, bodi hiyo iliweza kuziteketeza tani 5.48 za
vyakula visivyofaa kwa binadamu sambamba na kumfikisha kwenye vyombo
vya sheria mfanyakazi mmoja anayedaiwa kutupa dawa kinyume na
taratibu.
Kuhusu chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), katika hospitali ya Mnazi
Mmoja, waziri huyo alisema wodi hiyo imefanyiwa matengenezo makubwa
ambapo imewekewa vifaa mbali mbali.
Alisema miongoni mwa vifaa vilivyowekwa katika wodi ya ICU ni pamoja
na ‘monitors’ sita kwa ajili ya kuangalia viashiria muhimu vya
mgonjwa, mashine mbili za kumsaidia mgonjwa kupumua, mashine za
kuangalia ndani ya mwili, mashine ya kuangalia damu.
“Mafanikio ya kazi hii yanatokana na mchango mkubwa wa Baraza lako
tukufu pale lilipoweka msisitizo kwa wizara na serikali kwamba ICU
lazima ijengwe bila ya kushirikisha msaada kutoka nje,” alisema waziri
huyo.
Waziri Duni alisema hospitali ya Mnazi Mmoja inakabiliwa na changamoto
kadhaa ikiwemo uhaba wa wataalamu na kutoa wito Wazanzibar kurudi
nyumbani kufanyakazi kwenye hospitali za Zanzibar.
Akizungumzia vita dhidi ya maradhi ya malaria, waziri huyo alisema kwa
ujumla ugonjwa huo visiwani hapa unaendelea kudhibitiwa na kibakia
chini ya asilimia moja ya wagonjwa.
Waziri Duni aliwaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa wagonjwa wa
Zanzibar wanaopelekwa nje kwa matibabu wanaigharimu fedha nyingi
ambapo kwa mwaka 2010/2011 kiasi cha shilingi 906,295,038 zilitumika
kwa matibabu ya wagonjwa hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Baraza la
Wawakilishi ya Wanawake na Ustawi wa Jamii, Amina Idd Mabrouk, alisema
zipo taarifa za ukusanyaji mapato katika wizara hiyo zinafishwa.
Mwenyekiti huyo alisema wizara hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa
ikiwemo kuondoka kwa wataalamu wa afya na kutaka utafiti ufanywe ili
kujua mahitaji yao.
Kabla ya kuhitimisha kusoma bajeti hiyo waziri huyo aliliomba baraza
hilo kuidhinisha jumla ya shilingi 40,216,205,000 kwa matumizi yote
kwa mwaka wa fedha 2012/2013
Jambo la msingi ktk kutatua tatizo la uhaba wa wataalamu ni kuimarisha chuo chetu cha afya Mbweni.
ReplyDeleteMimi naamini wengi kati ya wataalamu wanaokimbilia nje ni wale ambao wamesomea nje na sio wale wa muhimbili au mbeni.
Zaidi ya yote hayo SMZ lazma iwe 'serious' ktk kuingia mikataba ya kusomesha madaktari, huwezi kumsomesha mtu kwa milioni 70 halafu'kakimbia' w'nchi hawatakuelewa!
Suala hapa ni sheria na uzalendo mbona kule cuba hawakimbii au kuna maisha gani kule?