Habari za Punde

Jaji Makungu: Mahakimu simamieni haki

Na Khamis Amani 

 MAHAKIMU wa mahakama za mwanzo, wametakiwa kusimamia ipasavyo masuala yanayohusiana na ukiukwaji wa sheria ndogo ndogo (by laws), na kuhakikisha haki inatendeka kwa maslahi ya umma.

 Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, alieleza hayo huko Dunga, katika ufunguzi wa mahakama ya mwanzo ya Halmashauri ya wilaya ya Kati Unguja. 

 Jaji Makungu alisema kuwa, mahakimu wanapaswa kuwa waadilifu katika usimamiaji wa kazi zao za kuamua haki, na kuhakikisha maamuzi yao wanayoyatoa yanazingatia sheria bila ya kuegemea upande mmoja. 


 Alisema kuwepo kwa mahakama za mwanzo katika Halmashauri ni hatua muhimu ya kuipelekea huduma hiyo karibu na wananchi, pamoja na kuzipunguzia mzigo mahakama za Mwanzo ziliopo katika mahakama za kawaida.

 "Mahakama za kawaida zilizopo zinashughulikia masuala ya jinai na ya madai kwa mujibu wa uwezo wa mahakama ulivyo, lakini kwa kuwa mahakama hii ni maalumu itakuwa inashughulikia masuala maalumu yanayohusiana na Halmashauri husika pamoja na sheria zinazosimamiwa na Halmashauri", alisema. 

Alifahamisha, lengo la kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni kutoa haki katika mashauri yanayopelekwa mbele yake, hivyo watoaji wa haki hizo wanapaswa kuwa waadilifu katika utekelezaji wa haki hizo.

 Katika hafla hiyo Jaji Mkuu alionesha kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kuanzisha mahakama hiyo, ambayo itaweza kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

 Aidha Jaji Mkuu alielezea matumaini yake kuwa kesi zote zitakazofikishwa katika mahakama hiyo hazitochukuwa muda mrefu kumalizika, kutokana na kesi hizo ni maalumu, na hizitakuwa na usumbufu kwa wananchi kama ilivyo kwa mahakama za kawaida. 

 Pamoja na hayo, Jaji Mkuu alifahamisha kuwa Idara ya Mahakama ipo tayari kupeleka huduma za kimahakama kila panapohitajika, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

 Akimkaribisha Jaji Mkuu wa Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame, aliipongeza Halmashauri ya wilaya ya Kati Unguja, kwa kutekeleza kwa vitendo sheria za Tawala za Mikoa iliyopitishwa hivi karibuni katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

Alisema kuwa, utekelezaji wa sera hiyo utaweza kurahisisha maendeleo ya Halmashauri, na kuwepo kwa mahakama hiyo itakuwa ni kichocheo cha maendeleo hayo kwa kuwabana wakorofi wote wasiolipa kodi mbali mbali zinazowastahikia. 

 Hafla ya uzinduzi wa mahakama hiyo, pia ilihudhuriwa na Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar George Joseph Kazi, Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar Abraham Mwampashi, Mkuu wa wilaya ya Kati Unguja, mahakimu dhamana wa mahakama za mkoa na wilaya, pamoja na maofisa mbali mbali wa wilaya ya Kati na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.