Habari za Punde

Hutuba ya Waziri wa Fedha Zanzibar Aliyoitowa Siku ya Idadi ya Watu Wiki Iliopita.

TAARIFA YA MHESHIMIWA OMAR YUSSUF MZEE- WAZIRI WA NCHI (OR) - FEDHA, UCHUMI NA MIPANGO YA MAENDELEO WA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR KWA WANANCHI KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA IDADI YA WATU DUNIANI, TAREHE 11/7/2012.

NDUGU WANANCHI,

ASSALAAM ALEYKUM

Awali ya yote ni kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi, Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia kuweza kuifikia siku hii ya leo tukiwa hai na katika afya njema, furaha, amani na utulivu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume ya Mipango imeshiriki kikamilifu katika maandalizi ya Kitaifa juu ya maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani kwa mwaka 2012.

Ndugu Wananchi,
Kwanza kabisa napenda nianze kueleza kwa ufupi kwamba kila ifikapo tarehe 11 Julai, ya kila mwaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupitia wadau mbali mbali wanaohusiana na masuala ya Idadi ya Watu Duniani huungana na jamii ya Kimataifa kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuzungumzia na kuelimishana juu ya masuala ya idadi ya watu, changamoto na maendeleo kwa ujumla.

Kila mwaka UNFPA, Shirika la Idadi ya Watu Duniani hutoa kaulimbiu kwa mnasaba wa matukio muhimu yanayojitokeza katika mwaka husika. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI KWA WOTE” Kaulimbiu hii inaendana na lengo la melania la 5b lisemalo ifikapo mwaka 2015 “Huduma za Afya ya Uzazi kupatikana kwa wote” Mkutano wa Kimataifa wa Idadi ya Watu na Maendeleo Duniani (ICPD) ulofanyika Cairo Misri mwaka 1994 ulitoa wito wa upatikanaji wa huduma za Afya ya Uzazi kwa wote ifikapo mwaka 2015 ikiwemo uzazi wa mpango, uzazi salama na kinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza kama Ukimwi.

Ndugu Wananchi,
Suala la Idadi ya watu na kasi ya kuongezeka kwake ni miongoni mwa changamoto zenye athari katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi Duniani na hapa Zanzibar pia. Taarifa zinaonyesha kwamba Zanzibar hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1.3 millioni wanaongezeka kwa kasi ya asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo idadi ya watu katika kila kilomita moja ya mraba imefikia watu 496 mwaka 2011.

Sababu kubwa zinazochangia ongezeko hili la watu ni pamoja na kiwango kikubwa cha uzazi cha wastani wa watoto 5 kwa kina mama wenye umri wa kuzaa, kiwango kidogo cha matumizi ya njia za uzazi wa mpango, ndoa za mapema n.k.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya wa mwaka 2009/10, kiwango cha matumizi ya njia za uzazi wa mpango (Contraceptive Prevalence Rate – CPR) Zanzibar kimefikia asilimia 12.4, kiwango ambacho ni kidogo na hivyo kuchangia katika kuwepo kwa wastani mkubwa wa kuzaa hapa Zanzibar. Tanzania Bara CPR imefikia asilimia 27 ambayo pia bado haijakidhi haja inayokusudiwa.

Taarifa za Wizara ya Afya Zanzibar pia zinaonyesha kwamba bado kuna muamko mdogo wa matumizi ya njia za muda mrefu za uzazi wa mipango (long term family planning methods) ikilinganishwa na zile za muda mfupi. Hivyo jamii inahitaji kuielimishwa zaidi juu ya kuwepo na ubora wa njia hizo za muda mrefu katika kupanga uzazi salama kwa mama zetu. Taarifa za mwaka 2010 zinaonesha ni watu 3,390 ndio waliojitokeza kupatiwa njia za muda mrefu za uzazi wa mpango sawa na asilimia 3.9 ikilinganishwa na watu 84,414 ( asilimia 96.1) waliorodheshwa katika matumizi ya njia za muda mfupi za uzazi wa mpango.

Watu walio wengi wameorodheshwa kwenye matumizi ya sindano (asilimia 71) ikifuatiwa na vidonge (asilimia 19.4). Hivyo juhudi zaidi zinahitajika ili kudhibiti hali hii na hatimae kuwe na uwiano mzuri baina ya ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa uchumi.

Ndugu Wananchi,
Sambamba na kaulimbiu ya kila mwaka, mafanikio na changamoto katika kutekeleza sera ya idadi ya watu pia hufanyiwa tathmini katika kipindi cha mwaka uliopita. Naomba kuchanganua zaidi changamoto zinazoikabili kaulimbiu ya mwaka huu ili zifahamike na tuweze kuzipatia ufumbuzi sahihi.

Miongoni mwa changamoto zinazoikabili dunia hivi sasa katika eneo la Afya ya Uzazi ni upatikanaji wa vifaa kwa utekelezaji wa uzazi wa mpango katika kujikinga dhidi ya mimba zisizotakiwa. Kiasi cha wananchi 215 millioni ulimwenguni wenye nia ya kuzuwia kuzaa kwa muda au kufunga uzazi- mtu mmoja kwa kila watu sita mwenye umri wa kuzaa- anakosa huduma za uzazi wa mpango.

Zaidi ya wanawake 50 kwa kila nchi duniani wanalalamikia kutokupata msaada wa wauguzi au kuchelewa kusaidiwa wakati wa kujifungua . Hata hivyo katika nchi zinazoendelea wanawake wanaendelea kufa kwa kukosa huduma za afya ya uzazi. Vifo vya Mama wajawazito viko juu hasa kwa kina mama wenye umri mdogo au walio maskini.

Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa Tanzania na Zanzibar vifo vya Mama waja wazito na watoto bado ni kikwazo katika kuleta maendeleo na kupunguza umasikini. Serikali zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar kwa kupitia wadau wa afya ya uzazi wameweza kupunguza kiwango cha vifo vya uzazi ingawa sio kwa kiwango kinachotarajiwa kama takwimu zinavyojionesha: kwa Tanzania katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo ilikuwa 578 kwa kila akina mama waja wazito 100,000 hadi kufikia vifo 454 mwaka 2010. Kwa Zanzibar vifo vya mama vimepungua kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi vifo 279 mwaka 2009 kwa kila kina mama 100,000.

Kwa upande wa vifo vya watoto, taarifa zinaonyesha kwamba vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kwa Tanzania vimepungua kutoka vifo 68 mwaka 2004/05 hadi vifo 51 mwaka 2010. Kwa Zanzibar kutoka vifo 61 mwaka 2004/05 hadi vifo 54 mwaka 2010 kwa kila watoto 1000.

Vifo chini ya miaka mitano kwa Tanzania navyo pia vimepungua kutoka vifo 112 mwaka 2004/05 hadi vifo 81 mwaka 2010 kwa kila watoto 1000. Kwa Zanzibar vifo vimepungua kutoka 101 mwaka 2004/05 hadi vifo 73 mwaka 2010 kwa kila watoto 1000.

Upungufu wa vifo vya mama waja wazito na watoto unatokana na juhudi kubwa inayofanywa na Serikali kwa kuimarisha huduma za afya, zikiwemo huduma za chanjo kwa akina mama wenye umri wa kuzaa na watoto ikiwa ni pamoja na chanjo za pepo punda, chanjo za shurua na ugonjwa wa kupooza kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Juhudi nyengine ni pamoja na wafanyakazi kupatiwa mafunzo mbali mbali yakiwemo ya huduma ya mtoto mchanga, mafunzo juu ya njia mbali mbali za uzazi wa mpango, huduma ya kuharibu mimba na uzuwiaji maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kusogezwa huduma za afya ya uzazi karibu na jamii kwa siku maalum.

Taarifa za mwaka 2012 kutoka wizara ya Afya Zanzibar zinaonesha kwamba asilimia 92 ya watoto chini ya miaka mitano wamepatiwa chanjo ya polio, asilimia 95 wamepatiwa matone ya Vitamin A na asilimia 94.2 wamepatiwa dawa za minyoo.

Juhudi hizi zinazochukuliwa na Serikali zimesaidia sana kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wake ambapo vifo vimepungua na wastani wa umri wa kuishi kwa mzanzibari umeongezeka hadi kufikia miaka 60 kwa mwaka 2011.

Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa changamoto zinazojionesha waziwazi katika eneo la afya ya uzazi ni kuolewa watoto wa kike katika umri mdogo na pengine kabla ya kumaliza masomo yao ya sekondari, kuongezeka kwa hali ya kinamama kujifungulia majumbani imekua pia ni mojawapo ya changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

Kutokana na changamoto hizi, naomba nichukue nafasi hii kutoa wito maalum kwa jamii kwamba ni vizuri tukawaozesha watoto wetu kati ya umri wa miaka 20 na kuendelea na ni vyema kuwasubiri wamalize masomo yao kwani elimu ni ufunguo wa maisha. Pia ningeshauri jamii na akinamama kujenga utamaduni wa kujifungulia hospitali ili kuepusha matatizo yanayoweza kutokea wakati wa kujifungua kwa vile Hospitali kuna vifaa na Madaktari wa kuyakabili matatizo ya dharura (emergency) kinyume na nyumbani. Aidha nashauri wizara ya afya kupanua huduma za jamii kwa kuwafata akina mama kwenye maeneo yao badala ya kuwasubiri kuja hospitali au vituo vya afya. Zoezi kama hili ni zuri, kwani kuna nchi nyingi tu kama Ethiopia tayari wameanzisha huduma za namna hii na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi.

Changamoto nyengine ni wanawake wa vijijini na upatikanaji wa huduma za Afya ya Uzazi: Katika kipindi cha maadhimisho ya siku ya Idadi ya watu duniani inatupasa kuzungumzia kwa uwazi masuala ya Ukimwi, jinsia, afya ya uzazi katika fungamano la kujamiiana na kueleza uhusiano wa mambo hasa katika mazingira ya mwanamke wa kijijini. Tuhakikishe kwamba mwanamke wa kijijini anaweza kuzitetea haki zake za Afya ya Uzazi kwa kumuezesha kielimu kama ni hatua mojawapo ya kupunguza umasikini na njaa. Wanawake wa vijijini wako nyuma katika utekelezaji wa malengo yote ya melania. Mathalan katika nchi zilizoendelea mwanamke mmoja kati ya wanawake watatu (3) anapata huduma ya kabla ya kujifungua “Prenatal care” kwa kulinganisha na asilimia 50 katika nchi zinazoendelea .

Ndugu Wananchi,
Huduma ya HIV/AIDS na Afya ya Uzazi, Ukimwi na matatizo yanayojitokeza katika kipindi cha ujauzito na kipindi cha kujifungua yanaongoza miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuzaa. Kutokana na ripoti ya mwaka 2007, juu ya utafiti wa Malaria na Ukumwi Tanzania, kiwango cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi Zanzibar ni asilimia 0.6 ambapo kwa mujibu wa takwimu hizi Zanzibar ni miongoni mwa nchi zenye kiwango kidogo cha maambukizi ya Ukimwi. Hata hivyo juhudi zaidi zinaendelea ili kuhakikisha kwamba kiwango cha maambukizi mapya ya Ukimwi kinadhibitiwa.

Njia kuu za maambukizi zinazojulikana kwa Zanzibar ni pamoja na kujamiana bila kinga na makundi makuu yaliyo katika hatari ya kupata ukimwi ni vijana wanaotumia madawa ya kulevya na wanaojidunga shindano, pamoja na wanawake wanaofanya biashara ya ngono. (Chanzo: Ant- drug Unit, Police HQ Zanzibar 2004).

Kwa hivyo ni vyema kwa makundi ya jamii kama viongozi wa dini, asasi zisizo za serikali, walimu maskulini na wazee majumbani kutoa elimu juu ya hatari ya matumizi ya madawa ya kulevya na biashara ya ngono . Kwani matendo yote haya ni chachu ya maambukizi ya Ukimwi na kifo.

Ndugu Wananchi,
Huduma ya mawasiliano pia ni suala la msingi linaloigusa kaulimbiu ya mwaka huu. Baadhi ya taarifa za huduma ya njia ya uzazi wa mpangilio zinahitaji kupanuliwa ili kuwafikia wateja husika. Vyombo vya Habari vitumike zaidi katika kuelezea umuhimu wa uzazi wa mpango ili kuondoa kasumba juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango. Aidha kupatikana kwa elimu ya ushauri nasaha kwa ajili ya kupunguza mimba za papo kwa papo ni jambo la msingi sana. Hata hivyo, katika juhudi ya kupanua huduma ya taarifa juu ya uzazi wa mpango, Kitengo Shirikishi cha Afya ya Uzazi na Mtoto, Wizara ya Afya kimezindua kitabu cha “Uislamu na Uzazi wa Mpango” ili kuieleza jamii ya kislamu kwamba Uislam unakubali uzazi wa mpango kwa lengo la kupunguza kasi ya ongezeko la Idadi ya Watu. Hivyo ni vyema kukisoma kitabu hichi na mafundisho yake tuyatumie kivitendo ili tulete mabadiliko ya kweli.

Kwa kuzingatia yote haya, siku ya tarehe 9/5/2012, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa makusudi alitangaza rasmi upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi kwa kina mama bila malipo yoyote katika Hospitali zote za Serikali kuanzia tarehe 01/07/2012. Aidha katika kuliunga mkono hili, Serikali kuanzia Bajeti ya mwaka huu 2012/13 imetenga fungu maalum kwa ajili ya huduma za afya, upatikanaji wa vifaa na madawa mbali mbali. Lengo na dhamira kuu ya kuchukuliwa uamuzi huu ni pamoja na kurahisisha upatikanaji huduma ya afya uzazi kwa kinamama, kupunguza vifo vya kina mama na watoto na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa ujumla . Aidha kupitia Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar, kanuni zinaandaliwa ili kina baba nao wapatiwe likizo (siku tano za kazi) la uzazi ili kumsaidia mama na mtoto aliezaliwa. Hatua hii itasaidia kuondokana na ile dhana kwamba suala la afya ya uzazi linamhusu mama pekee. Hatua hii inategemewa iwe chachu ya kuwashirikisha kina baba katika harakati zote za huduma ya afya ya uzazi na mtoto.

Ndugu Wananchi,
Kwa vile zoezi la kuhesabu watu lipo karibu sana, mwezi mmoja mbele yetu napenda kuchukua nafasi hii kuzungumzia suala la Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2012. Nawaomba wananchi wote wa Tanzania kutoa ushirikiano unaohitajika katika zoezi la kuhesabiwa kwani kujua idadi ya watu itasaidia Serikali kupanga mipango sahihi ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake. Zoezi la sensa litafanyika tarehe 26 Agosti, 2012, kwa hivyo wananchi tushirikiane na tuhamasishane kushiriki zoezi hili kwani kukosa kuhesabiwa mtu mmoja kutapoteza malengo yaliyokusudiwa na mipango sahihi ya maendeleo ya nchi yetu.

Ndugu Wananchi,
Kwa kuhitimisha taarifa hii, napenda kusisitiza kwamba serikali kupitia wadau wa afya ya uzazi wanaendelea kuziimarisha huduma za uzazi wa mpango, Uzazi salama na afya ya uzazi kwa vijana, kuongeza upatikanaji wa huduma bora za dharura za uzazi, kuinua kiwango cha chanjo zote kufikia zaidi asilimia 90 kwa wilaya zote za Zanzibar.

Aidha kuimarisha na kupanua huduma za kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Lengo kubwa kwa huduma hizi ni kuimarisha afya ya mama na mtoto ambayo ndio nguzo ya rasilimali watu iliyobora, itayozalisha vizuri na hivyo kuinua kiwango cha ukuaji wa uchumi nchini.

Ndugu Wananchi,
Mwisho kabisa napenda nizipongeze Tume za Mipango zote mbili ile ya Tanzania na Zanzibar kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho ya siku ya Idadi ya Watu duniani kwa mwaka 2012. Aidha natoa shukrani zangu za dhati kwa shirika la Idadi ya Watu Duniani UNFPA kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha masuala ya maendeleo ya watu hapa nchini ikiwa ni pamoja na maandalizi ya sensa ya watu ya mwaka 2012 na pia maadhimisho haya ya siku ya idadi ya watu duniani.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.