Na Mwandishi Wetu
TUME ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi
kuhusu malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa imeweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaotoa
maoni katika mikutano yake inayoendelea katika mikoa minane na kuwaomba
wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano inayoiitisha kutoa
maoni yao kwa uhuru na uwazi.
Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid alisema Tume
ingependa kupata maoni ya kila mwananchi na hivyo haiwezi kuweka ukomo kwa
wananchi kutoa maoni katika mikutano inayoiitisha.
Ufafanuzi wa Tume hiyo unafuatia taarifa kupitia
vyombo mbalimbali vya habari zikinukuu baadhi ya wananchi wakilalamika kuwa tume
hiyo imeweka kikomo cha idadi ya maswali
na watu wanaotakiwa kutoa maoni yao katika mikutano ya kukusanya maoni ya
wananchi.
Taarifa hizo ziliongeza kuwa tume hiyo imekuwa
ikitoa nafasi kumi tu kwa wananchi wanaopaswa kuuliza maswali yasiyozidi kumi
katika mkutano mmoja na kwamba, katika baadhi ya Wilaya, ikiwemo Biharamulo
yenye kata 15, ni kata sita tu ndizo zilizofikiwa na tume.
“Katika baadhi ya Wilaya, kama Kusini Unguja na
Bahi mkoni Dodoma, tume imelazimika kuongeza muda wa kupokea maoni ya wananchi
na wakati mwingine kuongeza idadi ya mikutano hadi kufikia mitatu badala ya
miwili kwa siku. Hatua hizi zinalenga kutoa fursa zaidi kwa wananchi kutoa
maoni yao,” alisema Assaa katika taarifa yake kwa vyombo habari.
Kuhusu mikutano iliyofanyika wilayani
Biharamulo, Assaa alisema Tume ilipanga na imefanya mikutano sita kuanzia Julai
2 hadi 4 Julai, na jumla ya wananchi 267 walitoa maoni yao kwa mdomo na
wananchi wengine 265 walitoa maoni yao kwa maandishi.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, vituo ambavyo
mikutano hiyo ilifanyika ni Kelenge, Movata, Nyamigogo, Runazi, Nyakanazi na
Biharamulo mjini.
“Katika mikutano hiyo na mikutano mingine yote tume
haikuweka na haitaweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaopaswa kutoa maoni,” alifafanua Assaa na kuongeza kuwa Tume inatambua kuwa
wananchi wana shauku kubwa ya kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya.
Hata hivyo, Katibu huyo alisema kuwa ingawa tume
ingependa kumfikia kila mmoja mahali alipo, jiografia ya nchi na muda ambao tume
imepewa, jambo hilo halitawezekana na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi
katika maeneo ambayo tume itafanya mikutano kama ratiba iliyotolewa
inavyoelekeza.
Akifafanua kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya kata
hazitafikiwa na tume, Assaa alisema tume haikupanga ratiba ya mikutano ya
kukusanya maoni kwa kuzingatia kata, bali imepangwa kwa kuzingatia eneo ambalo
linaweza kujumuisha wananchi kutoka zaidi ya kata moja.
Pamoja na kutoa maoni yao kupitia mikutano, tume
pia imewaomba wananchi kuendelea kutumia fursa nyingine kuwasilisha maoni yao kwa
njia ya tovuti ya tume (www.katiba.go.tz), barua pepe (maoni@katiba.go.tz) au
kwa njia ya posta kupitia tume ya mabadiliko ya katiba.
Tume ya mabadiliko ya katiba ilianza kufanya
awamu ya kwanza ya mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa minane
Julai 2 mwaka huu na inatarajiwa kumalizika Julai 30.
Mikoa
hiyo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga
na Tanga.
No comments:
Post a Comment