Na Hafsa Golo
HALI ya utata imejitokeza katika kijiji cha Bwejuu kati ya wanakijiji na Jeshi la Polisi kufuatia kuchukuliwa kwa eneo la wakulima ambalo litatumiwa na jeshi hilo kwa ujenzi wa Chuo cha Mafunzo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Bwejuu Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo kijiji cha Bwejuu, Badru Simai Makame alisema kuwa zimekiukwa taratibu za msingi kwa jeshi la polisi kuwepa eneo hilo kwani hawakushirikishwa kikamilifu.
Alisema kuwa ikiwa wao ni viongozi na wasimamizi wa kijiji hicho hivyo wanaungana na kilio cha wakulima kuwa hawakutendewa haki katika utoaji wa eneo hilo ambalo ni tegemeo katika uendeshaji wa maisha yao ya kila siku.
"Sisi ni wasimamizi wa wananchi niwajibu wetu kusimamia haki zao na jeshi hilo halikutenda haki kwani uchukuzi haukuwa na taratibu zenye kufahamika vizuri walichukuwa eneo bila ya ridhaa ya wananchi", alisema.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi wamekiuka taratibu kwani awali wazee wa kijiji hicho walitoa ridhaa ya kujengwa kituo kidogo cha askari pamoja na nyumba ya kukaa, lakini si kulichukua eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha mafunzo yao.
Alifahamisha kuwa eneo hilo ni muhimu na ni tegemeo kubwa kwa wakulima katika maisha yao ya kila siku huku wengine wakiwa tayari wamepanda miti yao ya kudumu.
"Ardhi hivi sasa ni mali si ichukuliiwe kiholela holela kwani ardhi haizuidi ila binadamu wanotumia ndio huzidi siku hadi siku”, alisema mwenyekiti huyo.
Kwa upande wa katibu wa baraza la wakulima wilaya ya Kusini Ali Dawa Simai, amekemea uchukuliaji wa eneo hilo kwani na kueleza kuwa haki haikutendeka.
"Eneo hilo lina mivinje haipungui 30, minazi 600, midimu 400, miembe 60, na ndani yake mnashamba la mibaazi na halipungui hekari zaidi ya 3, hii ni hasara kwa wakulima”,alisema.
Nae sheha wa shehia ya Bwejuu Suleiman Hassan Hassan alikanusha juu ya kuwepo hali hiyo na kueleza kuwa eneo hilo limetolewa na uongozi wa wa Bwejuu ambapo zilikutana kamati za masheha pamoja wazee wa mji na kupitisha uamuzi wa kutoa eneo hilo.
Alisema kuwa awali walikosea walitoa eneo la mwitu wa hifadhi wa kijiji baada ya kutafakari umuhimu wa thamani ya mwitu huo ndipo wakaamua kutoa eneo hilo ambalo lilikuwa halina thamani ya mazao kama inavyodaiwa na baadhi ya wakaaji wa kijiji hicho.
"Tulipowapa hapakuwa pamelimwa na wananchi wala hakuna miti yoyote, ila kuna mtu mmoja ambae kidogo mazao yake yameingia",alisema.
Kwa upande wa kamanda wa polisi wa mkoa wa Kusini Unguja, Agostino Ollomi, alisema polisi halijavamia eneo hilo bali waliomba kwa kufuata taratibu hasa wakizingatia wao ni dhamana wa kulinda raia mali zao.
Alisema kuwa kama kumejitokeza tofauti yoyote ni vyema pande zote mbili zifanye mazungumzo ya pamoja pia wananchi hao wapeleke malalamiko yao kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar upatikane ufumbuzi.
"Eneo tumeomba na tumefata sheria hatukuvamia tu kama inavyodaiwa tumekabidhiwa kihalali, lakini kama kumejitokeza hitilafu au madai yawasilishwe kwa Kamishna ili yatatuliwe na sio kusema maneno ambayo hayana ukweli", alisema
No comments:
Post a Comment