IKIWA jana ni siku ya kwanza kwa wananchi wa mkoa wa Kusini Unguja kuanza zoezi la kutoa maoni juu ya uundwaji wa katiba mpya, wananchi wa Makunduchi wamependekeza Muungano ubakie.
Aidha mbali ya kutaka Muungano uendelee, pia wananchi hao wa Makunduchi wametaka uwepo utaratibu utakaohakikisha Rais wa Zanzibar anakuwa na hadhi yake kama Rais wa nchi.
Wananchi hao walieleza hayo jana kwa wakati tofauti wakati wakitoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya kupatikana kwa katiba mpya katika kijiji cha Mzuri na Mtende katika Jimbo la Makunduchi wilaya ya Kusini Unguja.
Zoezi hilo la ukusanyaji wa maoni hayo liliongozwa na Mjumbe wa Tume hiyo kutoka Mohammed Yussuf Mshamba, na Dk. Salim Ahmeid Salim.
Wakitoa maoni yao kwa njia tofauti ikiwemo maoni kwa njia ya barua, wanananchi hao wengi wao walipendekeza Muungano wa serikali mbili ubakie wa serikali mbili, lakini kero za Muungano ziliopo ziondolewe na kumpa hadhi Rais wa Zanzibar.
Wananchi hao walieleza muundo wa Muungano uliopo sasa bado wanakubaliana nao ubakie kama ulivyo ila kero zitatuliwe na zisiwachwe zikiongezeka.
Walisema hawaoni haja ya kuona Muungano huo unavunjika kwa vile ulianzishwa na muasisi wa Taifa la Zanzibar Abeid Amani Karume ambao wao bado wanamuunga mkono.
Baadhi ya wananchi hao walieleza kero ziliopo katika Muungano hivi sasa ni kubwa, kiasi ambacho kimekuwa kikiwafanya viongozi wa Zanzibar kuonekana ndani ya Muungano kama hawana hadhi.
Mmoja wa watoa maoni hayo, alisema Muungano wa serikali mbili unahitaji kuona unabakia ila nafasi ya Makamu wa Rais iwe inashikiliwa na Rais wa Zanzibar, badala ya mfumo wa sasa wa kumtumia Makamu kutoka katika pande mbili za Muungano.
Kwa upande wake Khatibu Mwadini Ngondo, alisema Muungano wa sasa ubakie, lakini yajengwe mazingira ya Rais wa Zanzibar kuwa na hadhi yake hata pale anapoenda nje ya nchi.
Mwananchi mwengine, akitoa maoni yake alisema anataka Muungano ubakie kuwa katika mfumo wa serikali mbili, ila katika uteuzi wa nafasi za juu za uongozi hasa Rais, Makamu wa Muungano na Waziri Mkuu mmoja wao anakuwa Mwanamke.
Naye Abeid Ameir Razak, alisema ipo haja ya Muungano uliopo uangaliwe kwani imeonekana Zanzibar kutokuwa na maendeleo zaidi ikilinganishwa na Tanzania bara, kwani Wazanzibari bado hawajafikia milioni 2, 0000,000, lakini kipato chao kipo chini huku vyakula vikiwa na bei juu.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi hao walieleza kuwa hawakubaliani na mfumo wa sasa uliopo wa Muungano wa serikali mbili na ingekuwa busara serikali zikafikiria kuwapo kila upande uwe na serikali yake, na suala la Muungano liwe ndani ya mkataba.
Naye Hassan Ali Hassan mkaazi wa Mzuri, akitoa maoni yake alisema ni vyema Muungano kuona unabakia kuwa wa serikali mbili ila kero za Muungano zinahitaji kutatuliwa.
Naye Alhali Mwita Abdul, alisema ipo haja ya kuuangalia mfumo wa Elimu ya Juu kwa kuona Zanzibar inakuwa na Mamlaka yake na bara upande wake kwani utaratibu sasa tayari unaonesha kuwa na matatizo kama ilivyojionesha katika mitihani iliopita.
Kwa upande wa wananchi wa Matende, walieleza bado wanakubaliana na mfumo wa serikali mbili ila bado kunahitaji kuangaliwa baadhi ya mambo ambayo hayako sawa.
Ali Himid Ali, alisema anakubali mfumo wa sasa wa Muungano ubakie ila madaraka ya Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania ibakie kuwa ni suala la Muungano, pamoja na kumpa uwezo Rais wa Zanzibar awe na uwezo wa kuamua mambo yake pamoja na raslimali za nchi zibakie kila upande uwe na zake.
Naye Hassan Mohammed Hassan, alisema mfumo wa uchaguzi wa nafasi za Urais wa Zanzibar unahitaji kuangaliwa kwa kuona hachaguliwi Dodoma.
Akifungua mjadala kwa wananchi wa kijiji cha Mtende Mjumbe wa Tume hiyo, Dk. Salim Ahmeid Salim, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa katiba ni moja ya jambo muhimu kwani ndio sheria mama katika muongozo wa taifa.
Alisema jambo la kusikitisha kuona uundwaji wa Katiba ya mwanzo wananchi hawajawahi kushirikishwa lakini kwa mwaka huu serikali imeamua kuwapa muda wananchi kuchangia Katiba waitakayo.
Alisema jambo ambalo Tume hiyo italizingatia kuona kila mwananchi anapata nafasi ya kutoa maoni yao kwa uhuru na bila ya woga.
Nae Dk. Sengondo Mvungi akitoa salamu zake kwa wananchi hao alisema, katiba ni sehemu ya muongozo wa kuendesha maisha ya binadamu ili kubakia kuwa katika usalama jambo ambalo wananchi wanapaswa kuzingatia umuhimu wa kutoa maoni yao.
Alisema ni vyema wananchi wakaeleza ndoto zao ndani ya Tume hiyo na sio baadae kuanza kulalamika kama katiba haiwapi uhuru kupata mahitaji yao.
“Tume hii ni yenu na sio mseme Tume hii ya Rais Tume ni yenu mtatuambia nini mnataka kila mtu atapata muda kusema aseme atakalo kwa kutoa maoni yao kwani mwisho wa siku tutaeleza Wazanzibari wanataka nini” alisema Mvungi.
Nae Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mohammed Yussuf Mshamba, akitoa maelezo yake alisema katiba ya sasa imeonekana inamahitaji zaidi ambayo yanapaswa kufanyiwa mabadiliko na ndio maana wananchi wamepewa fursa kutoa maoni yao.
Alisema katiba ya sasa imeweza kuzingatia masuala ya utaifa, uzalendo, maadili, dola na malaka yake, ardhi, Muungano, Demokrasia, uhusiano na ulimwengu, mfumo wa utawala na ulinzi na usalama jambo ambalo wananchi bado wanalazimika kuyaangalia mambo hayo jinsi ya mfumo wanautumia sasa.
Zoezi hilo la ukusanyaji wa maoni litaendelea tena leo ambapo wananchi wa kijiji cha Kibuteni na Michamvi watapata nafasi ya kutoa maoni yao.
No comments:
Post a Comment