Habari za Punde

Raza Awataka Viongozi Kuwajali Wananchi


Na Khadija Khamis-Maelezo      

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza Hassanali amewataka viongozi wa Serikali kuangalia zaidi maslahi ya wananchi badala ya kujali maslahi yao binafsi.

 Aliyasema hayo leo wakati akichangia hotuba ya  Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati  kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2012-2013


Alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wamekuwa na matatizo ya kijamii lakini viongozi   wanajali zaidi maslahi yao kwa kuweza kupanga safari  nyingi  nje ya nchi jambo ambalo linachangia kutumia fedha nyingi za serikali.


“Watendaji wasifanye safari zisizokuwa za  lazima, tujali zaidi  maslahi ya wananchi wetu ambao wametuchagua kutuweka hapa, ” alisema Raza.

Raza alisema viongozi wanapaswa kujenga mashirikiano ili kuondoa kero za wananchi ambazo ni nyingi na bado hazijapatiwa ufumbuzi wa kutosha.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Mjimkongwe, Ismail Jussa Ladhu, akichangia bajeti hiyo alisema ujenzi holela wa makazi ya watu unasababisha Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kushindwa kuyafikia maeneo hayo linapotokezea janga la moto.

Aidha alisema kuna maeneo ya wazi ambayo wanapewa matajiri baada ya kutoa rushwa, hali inayowanyima watoto fursa yao ya msingi ya kucheza.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.