Habari za Punde

Shughuli ya Kuwabaka Wanawake Michezani yaendelea


Na Hafsa Golo
SIKU chacha tu mara baada ya kuripotiwa kujitokeza kwa vitendo vya ubakaji vinavyoambatana kwa njia za ushirikiana katika Manispaa ya mji wa Zanzibar, bado vitendo hivyo vinaendelea kushamiri.

Taarifa za karibuni kabisa zinaeleza kuwa watu wawili za zaidi wameripotiwa kubwaka baada ya kuzungwa kimazingara na kupandishwa juu ya varanda za nyumba za Michenzani na kufanyiwa unyama huo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake katika hospital ya Mnazi Mmoja, Dk. Msafiri Marijani alisema kwamba watu wawili wameripoti hospitali kwa uchunguzi baada ya kufanyiwa vitendo hivyo.


Alisema baada ya kuongezeka kwa matukio hayo wameamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili liweze kufuatilia kwa kina kuwepo kwa vitendo hivyo vinavyoendelea kujitokeza.

"Hali imekuwa si ya kawaida kwani mbali na wanawake wa mwanzo waliofika hapa  mwisho wa wiki, tumepokea  wengine wawili ambao wamekumbwa na tatizo hilo, hivyo kwa kushirikiana na wahusika tumetoa taarifa kwa jeshi la polisi kwa vile inawezekana ikawa  hawana  taarifa", alisema.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Azizi Juma Mohammed alithibitisha kupokea taarifa hizo kutoka wizara ya afya na kueleza kuwa wahusika waliokumbwa na tatizo hilo ambao baadhi yao wamefika katika kituo cha polisi Madema kuripoti.

Alisema kwa nyakati tofauti wamepokea taarifa juu ya kutokea tatizo ambapo maeneo yanayotumika kwa kufanyika vitendo hivyo ni juu varanda ya jumba namba tano ya Michenzani ambayo imeonekana kuwa hakuna kidhibiti cha kuingia kama yalivyo nyumba kama hizo.

Alisema vijana hao hufika katika maeneo hayo na kujitambulisha kuwa ni askari wa jeshi la  polisi au polisi jamii na hutumia njia ya kuwatisha na hata kuwabana kisheria kama wahusika wanakabiliwa na shitaka huku wakiongozana nae na hatimae huwafikisha juu varanda kwa kuwafanyia vitendo hivyo.

"Wanaokumbana na matokeo hayo baadhi yao wale ambao hukaa faraha na wanaume aidha huwa mke wa watu, au mwanafunzi kaaga kwao anaenda tushweni kwa kuogopa kujulikana ndipo anapoamua kuwafuata na kukutana na matatizo hayo na wengine hukutikana njiani", alisema

Aidha alisema mbali na kuwabaka pia huwanyanganya mali zao ikiwema dhahabu, simu na pesa na hata kuwapiga na kusababishia majeraha katika miili yao.

Mbali na hayo kamanda alisema kuwa watajipanga kuanzisha mikakati madhubuti ya kupambana na matukio hayo ikiwemo kuandaa operation katika maeneo yaliojitikeza vitendo hivyo na pia kuwatumia askari wainteligensia.

Hivi karibuni waziri wa Ustawi wa Jamii,Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto, Zainab Omar, aliwataka wananchi kuwa na mashirikiano ambayo yatasaidia kuondokana katika vitendo hivyo vya udhalilishaji na ukatili.

Alisema kuwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji vinawaathiri watoto na akina mama kiakili, kiafya na hata kimwili,hivyo alisema kuwa ili jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kunahitajika mashirikiano.

"Nakuombeni akina mama,akina baba na wazazi wenzangu kwa ujumla tuwe na mashirikiano madhubuti ambayo yatasaidia kuondosha hivi vitendo vya udhalilishaji ambavyo vinamuathiri mtoto na mzazi,kiakili,kiafya na hata kimwili,"alisema.

Hivyo alifahamisha kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, haikubaliani na vitendo hivyo na kuahidi kwamba, serikali itachukuwa hatua kali katika kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwa liikabili jamii.

1 comment:

  1. Hivi ni vitendo vya kinyama na aibu kubwa kwa jamii yetu, ambayo kila siku imekua ikijigamba kua na uchamungu.

    Jamii lazima ishirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama ili kumaliza aibu hii mara moja na wale wote watakaopatikana na hatia wachukuliwe hatua kali!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.