Habari za Punde

Wawakilishi Waitaka Benki ya Wanawake


Wasema Itawapunguzia Umaskini


Husna Mohammed na Hafsa Golo
WAJUMBE wa Baraza la wawakilishi wameipongeza serikali kwa azma ya kuanzishwa Benki ya wanawake Zanzibar, jambo ambalo litaweza kuwainua kiuchumi wanawake wa visiwa hivi.

Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, wajumbe hao walisema kuanzishwa kwa benki hiyo, itakuwa ni mkombizi kwa wanawake wa Zanzibar.

Mwakilishi wa nafasi za Wanawake, Farida Amour Mohammed, alisema kuanzishwa kwa benki hiyo kwa kiasi kikubwa itawakomboa wanawake ambao hali zao ni duni.


"Kuanzishwa kwa benki hiyo kwa kiasi kikubwa kutawawezesha wanawake kupata mikopo na kuaweza kuendesha shughuli zao kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujikomboa na uamasikini," alisema.

Nae Mwakilishi Kazija Kona wa nafasi za wanawake akichangia bajeti hiyo, alisema kuanzishwa kwa benki ya wanawake kwa kiasi kikubwa itawawezesha wanawake hasa wa vijijini kuwa na mwamko wa kuanzisha miradi ya kimaendeleo.

"Wakati umefika sasa kwa wanawake wa vijijini kuamka na kuanzisisha miradi jambo ambalo litawainua wanawake kiuchumi," alisema.

Hata hivyo, aliitaka Wizara husika kuwatupia jicho wanawake wa vijijini katika suiala zima la kuibua miradi hasa ikizingatiwa kuwa wamesahaulika katika kujiinua kimaendeleo.

Sambamba na hilo lakini Mwakilishi huyo aliitaka Wizara hiyo kiuwaangalia zaidi wazee ambao wamekosa matunzo kwa njia moja au nyengine.

Alisema wazee hasa walioko katika vituo vya kuwalelea wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na hivyo kukata tamaa ya maisha.

Nae Marina Joseph, Mwakilishi wa kuteuliwa aliwataka wanawake kujiweka tayari katika mikopo hasa kutokana na kuanzishwa kwa benki ya wanawake.

Alisema kwa kuwa benki hiyo imelenga katika kuwakomboa wanawake hivyo ni vyema kuitumia fursa hiyo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, akitoa ufafanuzi katika kikao hicho, alisema kuwa benki hiyo itaanzishwa ambapo kwa sasa serikali inaendelea na ushauri uelekezi ikiwa ni pamoja na fedha za kuanzishwa kwa benki hiyo.

"Kima cha chini cha kuanzisha benki zisipungue bilioni 15, hivyo serikali imeamua kutafuta ushauri uelekezi jambo ambalo halitaki kukurupuka kwa kuwa tunataka kufanya jambo kubwa na la maana, kufika miaka miwili mpaka mitatu si mwingi", alisema.

Aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuamini uanzishwaji wa benki hiyo, ambayo itaweza kuleta manufaa kwa wananchi wa Zanzibar, hasa katika kuwainua wanawake kiuchumi.

Nae Fatma Abdulhabib Fereji, akichangia bajeti hiyo, alisema nguvu ya pamoja inahitajika katika kutokomeza usafirishaji, ununuzi na utumiaji wa dawa za kulevya ambapo vijana ndio waathirika wakubwa wa dawa hizo.

Alisema kwa kuwa wizara hiyo inashughulikia vijana basi ni vyema kukabuniwa mkakati wa makusudi wa kukabiliana na tatizo hilo, ambalo limekuwa likiwasumbua vijana wengi kwa kujihusisha na dawa hizo.

Nae Juma Duni Haji, Waziri wa Afya, akichangia bajeti hiyo alisema vitendo vya udhalilishaji vimekuwa ni tatizo kubwa hapa Zanzibar, jambo ambalo limekuwa likiumiza vichwa vya watu wengi.

Aliwataka wananchi kuwa macho, kutokana na kuibuka vitendo vya hadaa kwa wabakaji dhidi ya wanawake na watoto.

Wawakilishi wengi waliochangia bajeti hiyo, walikerewa na vitendo vya udahalilishaji wa kijinsia hasa tendo la ubakaji ambalo limeshamiri katika visiwa hivi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.