Na Bakar Mussa, Pemba
FAMILIA a 7 za wananchi wa kisiwa cha Pemba,
ambao walikimbilia nchini Somalia na kuhifadhiwa katika kambi za wakimbizi , zimewasili
kisiwani Pemba na kuunganishwa na familia zao
baada ya kupotea kwa muda wa miaka 12.
Familia hizo ni miongoni mwa familia 12 za
wananchi wa Zanzibar , ambao walikuwepo nchi Somalia kama wakimbizi tokea mwaka
2000, na kuamuwa kurejea makwao ilikuungana na ndugu zao ambapo familia sita zimebaki
kisiwani Unguja.
Wakiwasili katika bandari ya Mkoani Pemba na
kupokelewa na jamaa zao na maafisa
mbali mbali wa serikali na vyombo vya
dola huku wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba , Meja (mstaafu) , Juma
Kassim Tindwa, walisema kwamba wamefarajika na kufurahishwa sana kwa kitendo
hicho kilichofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa ( UNHCR).
Walieleza kwamba fursa hiyo walioipata walikuwa
wana isubiri kwa hamu na kwamba sasa imewafikia na hivyo wamejiona kama ni watu
ambao wamezaliwa upya , kwa vile wamewasili wakiwa na familia nyengine ambazo
walizipata wakiwa huko.
Mmoja kati ya wananchi hao, Ali Jaffar Othman
(46)mzaliwa wa Mchanga Mrima Ole, katika wilaya ya Wete, aliliambia gazeti hili
kwamba amefarajika sana kuona kwamba amerejea katika nchi yake na ana imani
kuwa Zanzibar kwa sasa imeshatulia.
“ Najisikia raha sana leo, nikiwa katika nchi
yangu naamini sasa imetulia ni tafauti na vile tulivyoiacha,” alisema.
Mwananchi mwengine, Ahmed Khatib Omar (30)
mzaliwa wa Shengejuu , Wilaya ya Wete, alisema pamoja na kwamba alikuwa
anawasiliana na jamaa zake , lakini anajisikia raha zaidi baada ya kuungana nao
tena baada ya miaka 12.
Wakati alipokimbilia Somalia alikuwa na umri wa
miaka 18.
Ali Haji Ali (37) mzaliwa wa Mtoni Chake
Chake, alisema anajisikia yuko katika
hali ya furaha kubwa kwa kufika nchini kwake kwani alikuwa ana wasiliana na
jamaa zake kwa njia ya simu tu.
“Mimi najihisi kama nimezaliwa upya kwa vile
nimefika kisiwani Pemba na kupokelewa na jamaa zangu nikiwa na afya njema. Ila
nasikitika sana kwa sababu baba yangu amefariki wakati mimi nikiwa Somalia,
sikupata nafasi ya kumzika,” alisema.
Alawi Ali Abdalla (36) mzaliwa wa Kisiwani kwa
Bint Abeib, katika Wilaya ya Wete-Pemba, alisema kuwa: “mimi sijisiki raha sana
mpaka pale nitakapoungana na familia yangu ilioko kisiwani na kunipokea hapo
nitajisikia na kujiona niko nchini mwangu”.
Nae , Rashid Abdalla Said (32) mzaliwa wa Msingini Chake Chake aliishukuru
Serikali ya Tanzania kwa mashirikiano makubwa na serikali ya Somalia hali
iliyowafanya warudi nyumbani wakiwa salama.
Aliomba kuhakikishia usalama wao ,na iwapo
watapatiwa hilo basi watakuwa na ushawishi mkubwa kwa wale wenzao ambao kwa
sasa hawajaamuwa kurejea Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Meja (mstaafu) ,
Juma Kassim Tindwa, akiwapokea wananchi hao aliwataka warejee makwao kwa amani
na utulivu na waendelee kushirikiana na familia zao katika ujenzi wa taifa.
Alisema: “ Zanzibar mulioiacha sio hii iliopo
sasa , imebadilika kwa kiasi kikubwa , ina utulivu na iko shwari kila mmoja
nalitenda analolitaka alimradi havunji sheria, hivyo navyi karibuni na
musijiingize katika makundi ambayo hayaitakii mema Zanzibar”.
Alisema mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe , na
mvunja nchi na mwananchi mwenyewe hivyo wawe tayari kuishi kwa amani na kujiletea maendeleo na kuwa tayari
kushirikiana na wananchi wengine kwa ajili ya kuilinda na kuitetea amani iliopo
kwani ndio njia pekee ya kuleta maendeleo ya haraka.
Afisa wa Shirika linalowahudumia wakimbizi kanda ya Somali na Kenya, Bruno Geddo ,
alisema kuwa anashukuru sana kuona kwamba tatizo la wakimbizi hao kuwarejesha
makwao limepatiwa ufumbuzi na sasa wamesha wafikisha katika familia zao ambazo
wamepoteana nazo kwa muda mrefu .
Alisema kuwa UNHCR, inaamini kuwa wananchi hao
ambao wamerejea makwao watapokelewa na jamaa zao na kushirikiana nao kwa kila
hali na juhudi za kuwarejesha wale ambao wamebakia huko Somalia zitaendelea.
Alisema UNHCR itazipatia familia hizo chakula
kwa muda wa miezi minne pamoja na mtaji wa kuanza maisha mapya.
Nae Msaidizi Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, Abdi Bulushi Juma,
alisema kuwa wakimbizi hao wamekubali kwa hiari yao kurejea nyumbani baada ya kuweko Somalia kwa muda mrefu.
Wakimbizi hao wamewasili kisiwani Pemba, wakiwa
na familia zao wakiwemo wake na watoto ambao waliwapata wakiwa Somalia miongoni
mwao wakiwa wanawake wa Kisomali.
No comments:
Post a Comment