Habari za Punde

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Yatowa Mafunzo kwa Mawakala wa Uchaguzi wa Wilaya ya Mjini Unguja na Kusisitiza Amani katika Uchaguzi Mkuu 2025

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imefungua mafunzo ya siku moja kwa Mawakala wa Uchaguzi, ikisisitiza umuhimu wa utendaji wenye weledi, uwajibikaji na kuimarisha amani kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mjumbe wa Tume hiyo Mhe.Halima Mohammed Said, alisema jukumu la Mawakala wa Uchaguzi ni kubwa, kwani wanahusishwa moja kwa moja katika utekelezaji wa majukumu muhimu ya Tume katika vituo vya kupigia kura.

"Mnapaswa kuijua nafasi yenu kwa Tume, na mnatarajiwa kuwa walimu wazuri kwa wenzenu katika ngazi za vituo na kila mmoja wenu atumie nafasi yake kufikisha elimu, taarifa sahihi na kuhimiza amani kabla na baada ya Uchaguzi,” alisema.

Aidha, Tume imeeleza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu ya Wapiga Kura na majukumu mengine ya Uchaguzi, yote kwa mujibu wa Sheria na miongozo ya Uchaguzi.

Tume imesisitiza kuwa Mawakala ni wadau wakubwa katika masuala ya Uchaguzi na demokrasia, kwani wana mchango mkubwa katika kuhakikisha Uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa amani.

“Ni muhimu kufahamu kuwa Mawakala wa Uchaguzi ni sehemu ya ujenzi wa demokrasia, wanaweza kusaidia kuhakikisha Uchaguzi unafanyika kwa uwazi na utulivu kwa kila hatua,”

Tume pia imetoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi kuendelea kushirikiana ili kufanikisha maandalizi ya Uchaguzi wa mwaka 2025.

“Matayarisho kwa ajili ya Uchaguzi wa 2025 yanaendelea, hivyo tunawaomba wadau wetu tushirikiane katika kufanikisha hili kila mmoja wetu kwa nafasi yake,”

Mafunzo hayo ya siku moja kwa Mawakala wa Uchaguzi wa Wilaya ya Mjini yamefayika Makao Makuu ya Tume iliyopo Maisara Wilaya ya Mjini Unguja.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.