Habari za Punde

ARDHI CLINIC CHALINZE

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Bwana Rugambwa (Kulia) akimpa maelezo Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Issa Ndemanga katika uzinduzi wa Kliniki ya Ardhi Halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani tarehe 11/10/2025

Na Lusajo Mwakabuku – WANMM Chalinze.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe Shaibu Issa Ndemanga, amewaasa wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani hususan Halmashauri ya Chalinze kuacha tabia ya kuuza maeneo yao kwa bei isiyoendana na soko.

Ndemanga ameyasema hayo leo 11/10/2025 wakati akizindua rasmi Kliniki ya Ardhi inayoendeshwa katika Halmashauri ya Chalinze ikiambatana na maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja katika uwanja wa Ofisi za Halmashauri hiyo mkoani Pwani.

Amewataka wananchi wa Chalinze kujitokeza kwa wingi siyo kwa ajili ya kupata hati peke yake bali pia kupata elimu juu ya ardhi ili watambue thamani halisi ya maeneo yao.

“Naomba kuwaambia wazee wangu mliopo hapa na wengine muwapelekee habari hii, acheni kuuza maeneo yenu kiholela. Hii Pwani yote sasa hivi soko linaendelea kukua kila siku, kumbukeni Dar es salaam imeshajaa na sasa inapumulia huku kwetu, kuna nafasi nyingi za uwekezaji na utajiri wa kutosha iwapo mtaitumia rasilimali hii ipasavyo” Alisema Mkuu wa Wilaya huyo.

Aidha, Mhe. Ndemanga ameongeza kuwa, iwapo wapo wakazi wenye maeneo wanaodhani hawawezi kuyaendeleza basi wafike katika Ofisi za Ardhi au kupitia Kliniki inayoendelea ili waweze kupatiwa elimu ya thamani ya maeneo yao ili   waweze kuuza kwa bei sahihi ama kuingia ubi ana wawekezaji huku wakiendelea kuyamiliki maeneo yao.

“Kuna mzee mmoja hapa Jirani nimeshuhudia Watoto wake wanakuja kulalamika kuwa kauza eneo kwa shilingi Laki Moja na Nusu! Hii ni fedha ndogo sana ambayo haiendani na thamani ya eneo hasa wakati huu ambapo nchi yetu imefungua milango kwa wawekezaji na hapa kwetu ni sehemu muhimu kwa sekta hiyo” aliongeza Ndemanga.

Akisoma taarifa ya utangulizi ya Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Chalinze Bw. Deo Msilu alisema huduma ya Klinik ya Ardhi katika Halmashauri ya wilaya ya Chalinze inayoendeshwa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Kamishina wa Ardhi msaidizi Mkoa wa Pwani ilianza tarehe 7/10/2025 na itafanyika kwa wiki mbili.

Akiongelea zoezi la Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi katika Halmashauri ya Chalinze lililoanza rasmi mnamo tarehe 27/06/2024, Bw. Msilu alisema Kliniki hii inaendeleza zoezi hilo ambalo hadi kufikia tarehe 30/3/2025, Kata tatu za Bwilingu, Pera na vigwaza jumla ya vipande vya ardhi 24,730 vimeshatambuliwa huku viwanja 23,936 vikiwa vimepimwa.

"Zoezi hilo limekuwa na mwitiko mkubwa sana kwa wananchi ambao walikuwa na kiu ya muda mrefu ya kupimiwa maeneo yao, wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama za upangaji na upimaji" amesema

Kwa mujibu wa Bw. Msilu, zaidi ya wananchi 500 hadi sasa wamehudumiwa kupitia kliniki hiyo aliyoieleza kuwa imerahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma za kisekta kwa wananchi zikiwemo utoaji wa elimu ya ardhi, upokeaji wa kero za wananchi, utatuzi wa migogoro, umilikishaji na ugawaji wa hati miliki za ardhi zao ikitumia mfumo wa kisasa wa eArdhi ambao umerahisisha utendaji kazi za upangaji, upimaji na umilikishaji.
Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo akikabidhi Hati kwa Mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata huduma katika Kliniki Hiyo.
Baadhi ya wananchi wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa wa Kliniki ya Ardhi Halmashauri ya Chalinze tarehe 11/10/2025 iliyoandaliwa kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja Mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.