WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuhakikisha Tanzania inakuwa na nguvukazi yenye ujuzi wa kisasa na inayoweza kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa.
Amesema lengo ni kuhakikisha nguvu kazi hiyo inakuwa na mchango katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema hayo leo Jumamosi (Oktoba 11, 2025) wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lilizofanyika katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Mafanikio ya taifa letu katika miaka ijayo yatategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa watu wake. Msingi wa maendeleo ya taifa letu ni watu wenye ujuzi, ubunifu, na maadili. Tuweke mbele elimu bora, ujuzi, ubunifu, na uzalendo kama silaha za kujenga taifa lenye ustawi, amani, na maendeleo jumuishi.
Amesema kuwa katika kuhakikisha Tanzania inaandaa nguvu kazi imara imetekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuanzisha Programu za Elimu ya Ufundi na Ujuzi (VET na TVET) kwa kupanua wigo wa vyuo vya VETA katika kila Wilaya na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya vitendo.
“Pia, Serikali imeanzisha Programu ya Taifa ya Maendeleo ya Ujuzi (National Skills Development Programme) inayolenga kujenga ujuzi kwa vijana katika sekta za kilimo, viwanda, teknolojia, nishatina huduma”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi, na vijana wa Tanzania kote nchini, kushirikiana katika kutekeleza kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa 2050
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Taasisi za biashara, viwanda, na mashirika binafsi kwa kushirikiana na taasisi za Serikali kuanzisha programu za mafunzo kwa vitendo maeneo ya kazi ili kukuza stadi za kazi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Daniel Mushi amesema kuwa Wizara inatambua mchango wa Sekta binafsi katika kukuza nguvu kazi ya Taifa kwa kutoa Elimu kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa ikiwemo ujenzi wa miundombinu, programu za mafunzo ya vitendo na utafiti pamoja na kuboresha taasisi binafsi z elimu
“Pia Serikali imeendelea kuongeza fedha kwa ajili ya kuboresha mifumo wa upangaji wa utoaji mikopo ya Elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayetoka katika familia isiyo na uwezo anapata fursa sawa ya kujifunza”
Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Prof. Alexander Makulilo amesema kuwa lengo la kongamano hilo kukuza na kuenzi urithi wa mwalimu nyerere katika maendeleo ya Rasilimali watu, kubaini njia za kimkakati za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi inayoweza kuendana na mahitaji ya Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na kukuza majadiliano baina ya wadau kuhusu sera na ubunifu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, OKTOBA 11, 2025
No comments:
Post a Comment