Na Rose Chapewa, Morogoro
WAKULIMA 30 kutoka katika kijiji cha Konga kata ya Mzinga Manispaa
ya Morogoro wamepata mafunzo mbalimbali ya kilimo hai, ikiwemo namna ya
kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa, pamoja na kutengeneza dawa
zitokanazo na mimea.
Mafunzo hayo ambayo yaliyokuwa ya siku kumi yalitolea na
Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na Kilimo Endelevu Tanzania
SAT mkoani Morogoro, huku lengo likiwa ni kutoa mafunzo hayo kwa wakulima 100
hadi kumalizika kwa mwaka huu.
Akizungumza na Zanzibar Leo, Mkurugenzi wa Shirika hilo Jeneth
Maro alisema lengo la mafunzo hayo ni kuchangia kuongeza uhakika wa
chakula na kupunguza umasikini kwa kutoa
na kuelekeza njia nzuri ya teknolojia
katika kilimo.
Alisema pia kutoa mwongozo na ushirikiano kwa wakulima, ili
kuendana katika njia ya kilimo endelevu na kuweza kuongeza uzalishaji wa
mazao kwa kutumia mbinu ambazo ni rafiki wa mazingira.
Aliyataja masomo waliyofundisha kuwa ni kilimo endelevu, kanuni za
kilimo hai, rutuba ya udongo, kupandikiza miche, mboji, na mboji iliyoboreshwa
(double super), namna ya kutayarisha shamba ama bustani, kitalu na matunzo
yake.
Nyingine ni kilimo mseto, mtandazo, teknolojia ya EM, shamba
mfuko, teknolojia ya sukuma - vuta, bustani kichunguu, marafiki wa mkulimna,
chai ya samadi na mimea, kilimo cha mbogamboga, wadudu waharibifu,
magongwa,magugu na namna ya kuthibiti wadudu waharibifu, magonjwa na dawa
zitokanazo na mimea.
Mmoja wa washiriki aliyejitambulisha kwa jina la Abdu Kondo
alisema kutoka na mafunzo hoyo amejifunza kuepuka matumizi ya vyakula
vitokanavyo na mazao yaliyowekwa kemikali.
Alisema mafunzo hayo yamemwezesha kutambua athari za
utumiaji vyakula vyenye kemikali, na kwamba yanaathiri afya ya mlaji na
kuharibu mazingira, na kwamba kwa sasa atalima mazao ambayo hatatumia kemikali
wala kula vyakula vya aina hiyo.
Naye Mshiriki Pantaleo Martin alisema amejifunza namna ya kuandaa
dawa za mimea pamoja na mbolea, ambazo hazina kemikali na hazina madhara kwa
mlaji na kwamba kwa sasa hatatumia tena dawa za dukani.
Alisema amejifunza kuandaa dawa za mazao zenye kutumia miti ambayo
aliitaja baadhi kuwa alizeti pori,
papai na alovera, na kwamba atalima kwa kutunza mazingira ili kuhakikisha
yanakuwa endelevu.
Aidha Mkurugenzi wa shirika hilo
alisema, katika maonesho ya Kilimo Nane nane anatarajia kualika wakulima 150
kutoka katika meneo mbalimbali mkoani hapa.
Alisema lengo ni kusambaza kilimo endelevu kwa wakulima wengi
nchini kwa kuwa hawafahamu, ambapo wanatakiwa kujua athari zinazoendelea
kutokana na kilimo kinachotumia kemikali, ili wachukue tahadhari kunusuru
mazingira.
No comments:
Post a Comment