Na Mwantanga Ame
KAMATI ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi imesema itaifanyia uchunguzi michango ya walimu, wanafunzi, wanayoitoa kuchangia elimu kwa kile ilichoeleza kuwa hakuna utaratibu mzuri wa matumizi yake.
Mjumbe wa kamati hiyo, Nassor Salim Ali, alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi wakati wa kupitia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Mjumbe huyo alisema upo umuhimu wa kufanyika kwa uchunguzi huo kwani inaonekana michango hiyo ina mkono mwengine inakoingia kutokana na usimamizi wake kubakia chini ya wizara ya Elimu badala kuingia katika mfuko mkuu wa hazina Zanzibar.
Alisema licha ya kuwapo kwa ongezeko la mapato na vyanzo vipya vya fedha ndani ya wizara ya Elimu, lakini bado kuna malalamiko yanayoendelea kutokea juu ya matumizi ya fedha hizo na usimamizi wake unavyoweza kutoinufaisha serikali juu ya michango inayotolewa.
Mapato hayo alisema ni yale yanayohusu malipo ya walimu wanaosoma katika vyuo vya Ualimu, michango ya wajibu ya walimu wote wa Zanzibar, na michango ya wazazi maskulini.
“Pamoja na kuwa kuna sababu za kuonyesha kuwa fedha hizi hazifiki kwenye wizara moja kwa moja, lakini ukweli ni kuwa fedha zinachangwa na wananchi na zinaingia mikononi mwa wizara, Mhe. Spika Kamati yetu itahakikisha inafanya uchunguzi ili kubaini mwenendo mzima wa mapato hayo na kuhakikisha kuwa fedha hizo zinaainishwa katika mapato ya serikali”, alisema Mjumbe huyo.
Mjumbe huyo alisema wizara hiyo baada ya kubuni njia mbali mbali za kuongeza mapato imeweza kuonesha mafanikio ya kuongezeka mapato katika makisio ya bajeti kwa mwaka mpya wa fedha, kutoka shilingi milioni 15 hadi kufikia shilingi milioni 22.
Hata hivyo, kamati hiyo imeeleza kuwa nguvu zaidi zinahitajika ili wizara iweze kufikia zaidi ya kiwango cha asilimia 57 cha mwaka uliopita.
Akizungumzia juu ya suala la matumizi ya Chuo Kikuu cha SUZA kamati hiyo ilisema haijaridhika na fungu lililotengwa kwa Chuo hicho la shilingi bilioni 4.2 kwa hali ya chuo hicho hivi sasa sio ya kuridhisha na serikali isitegemee kama kutakuwa na ufanisi kama kunakuwa na bajeti isiyotekelezeka.
Akizungumzia juu Mamlaka ya Mafunzo ya Amali alisema kuna ruzuku inayotolewa na serikali na “Kodi ya Ushuru wa kuongeza ujuzi (SDL) ambayo hutozwa waajiri binafsi kwa lengo la kusaidia uendeshaji wa Mamlaka hiyo hadi sasa taarifa ,zake zinaeleza kuwa Wizara ya Fedha imekuwa ikipatiwa shilingi milioni mia tatu na hamsini kwa mwezi na TRA kupitia makusanyo yatokanayo na mapato hayo.
Kuhusu mishahara ya wafanyakazi katika Mamlaka hiyo, Kamati hiyo imesema imekuwa ikipata malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kwa Unguja na Pemba dhidi ya Wizara husika, kwa kutowapa mishahara mipya ambayo imedaiwa kutoingizwa kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
Alisema baada ya kulifuatilia suala hilo Kamati hiyo imebaini fedha hizo za mishahara kimsingi zimetumika kinyume na utaratibu na wamepatwa na wasi wasi juu ya udhibiti wa matumizi yanayofanywa katika fungu la mishahara mipya ya wafanyakazi wa Mamlaka hiyo, na pia wafanyakazi wa hawakufaidika na nyongeza ya jumla ya mishahara.
Naye Rashid Seif, Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani, akitoa mchango wake alisema ipo haja ya Wizara ya Elimu kuona inajipanga vyema kutambua mpango maaalum utaoweza kulimaliza tatizo la kukosekana kwa vikalio ili lisijirejee mwaka hadi mwaka, huku kukiwa na michango inayotolewa katika kukabiliana na tatizo hilo.
Mwakilishi wa Wanawake, Mtumwa Kheir, akitoa mchango wake alisema ipo haja ya serikali kuliangalia suala la matumizi ya skuli za masomo ya ziada kutokana na kuonekana huenda ikawa ni chanzo cha watoto wengi kupata mimba hiku wengine wakilawitiwa.
Alisema hiyo ni hatari inayohitaji kufanyia kazi kwa kina kwani matukio ya kulawitiwa kwa watoto wa kiume yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku jambo ambalo linatishia mustakbali wa watoto wa kiume wakiwa skuli.

No comments:
Post a Comment