Joseph Ngilisho, ARUSHA
MFANYABIASHARA aliyetambulika kwa jina la Joseph Ngisha (24) mkazi wa sakina Songambele, jijini Arusha anashikiliwa na polisi kwa kosa la kumuoa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, polisi pia inamshikilia baba mzazi wa mtoto huyo, Lemomomo Olokuto (42) mkazi wa Mto wa mbu kwa tuhuma za kumwoza mtoto wake akiwa na umri mdogo.
Alisema Ngisha alitiwa mbaroni Julai 18 mwaka huu majira ya saa 3:45 asubuhi nyumbani kwake baada polisi kupata taarifa za siri na kumkuta akiishi na mtoto huyo huku akiwa amembebesha ujauzito wenye umri wa miazi mitatu.
Kamanda Sabas alifafanua kuwa Ngisha alianza kumchumbia mtoto huyo baada ya kuacha kunyonya kwa mama yake na kwamba alipofikisha umri huo aliwafuata wazazi wake ili wampatie ridhaa ya kuishi naye, hata hivyo mzazi upande wa mama aligoma huku baba yake ambaye ni mtuhumiwa akiruhusu mtoto wake aolewe bila kupingwa.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa Ngisha baada ya kuona mama mzazi akipinga mtoto wake asiolewe, alimrubuni kuwa anakwenda kumsomesha skuli, kitendo ambacho hakukifanya na badala yake alikuwa akimwingilia kimapenzi na kumfanya kama mke.
Kamanda alisema kuwa taarifa za mtuhumiwa kuishi na mtoto huyo kama mke ziligunduliwa na majirani kwani mara nyingi alikuwa akimfungia ndani bila mtu kujua huku akiwaeleza baadhi ya jamaa zake kuwa ni mdogo wake.
Aidha alisema kuwa kwasasa hivi mtoto huyo yuko chini ya ofisi za ustawi wa jamii ambapo anachunguzwa kwamba ameathirika kwa kiasi gani, huku uchunguzi wa awali ukionesha kuwa mtoto huyo ameathiriwa kwa kupata ujauzito wa miezi mitatu ambapo kulingana na umri wake ni vigumu kuhimili maisha ya kuitwa mama.
Uchunguzi wa awali kutoka ndani ya jeshi la polisi unaonyesha kuwa Ngisha alimchukuwa mtoto huyo tangu mwaka 2010, ambapo alipohojiwa kwa mara ya kwanza alikataa kosa hilo hadi siku ya jana ndipo alipokiri kutenda kosa hilo.
Sabasi alisema kuwa kufuatia tukio hilo baba mzazi anashikiliwa na kuunganishwa na baba mkwe wake, na kwamba wote wawili watafikishwa mahakani kujibu tuhuma zianzowakabili baada ya jeshi la polisi mkoani hapa kukamilisha uchunguzi wake kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment