Na Mwantanga Ame
BARAZA la Wawakilishi Zanzibar limeahidi kuendeleza mahusiano na balozi za mataifa mbali mbali zilizopo nchini.
Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho, aliyasema hayo juzi jioni katika chakula cha futari kilichoandaliwa na Baraza hilo kwa wajumbe wa Baraza hilo, iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort ambapo hafla hiyo Balozi mdogo wa India mjini Zanzibar, Pawel Kumar alishiriki.
Spika Kificho, alisema Baraza la Wawakilishi linathamini sana mchango wa mabalozi ambao wapo nchini kwa ajili ya kuziwakilisha nchi zao na wanaahidi kuona uhusiano huo unaendelezwa.
Alisema suala la uhusiano wa kimataifa serikali ya Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikishirikiana na mataifa mbali mbali duniani na Baraza lake litaendelea kuthamini mchango wa mabalozi hao.
Alisema Baraza hilo litathamini mchango huo kwa kutambua umuhimu wa uhusiano wa kimataifa na kitendo cha ubalozi wa India kushirikiana katika chakula hicho ni sehemu ya kuongeza upendo kwa Taifa hilo na serikali ya Zanzibar.
Alisema India ni moja ya nchi rafiki kwa serikali ya Zanzibar kwa muda mrefu na Baraza hilo linaahidi kuwa litaendeleza uhusiano huo.
Pia Spika kificho aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kuzidi kushikamana kuona wanatekeleza majukumu yao vizuri ili kuifanya nchi kuwa na maendeleo zaidi.
Spika huyo aliwatakia wajumbe hao kumaliza vyema saumu ya mfungo wa ramadhani pamoja na kuwatakia sikukuu njema pamoja na wananchi wote.
Chakula hicho cha futari kilihudhuriwa na wajumbe mbali mbali wa baraza hilo wakiwemo Mawaziri, wafanyakazi wa Baraza la Wawakilishi, Waandishi wa Habari na wageni waalikwa.
Waumini wa dini ya kiislamu hapa nchini wanaendelea na swaumu ya mfungo wa ramadhani ikiwa leo ni siku ya 23 tangu mwezi huo kuanza.
No comments:
Post a Comment