Habari za Punde

Maofisa utumishi wadaiwa kuichakachua mishahara. Wawakilishi wasema ni mtandao wa wizi

Na Mwantanga Ame
WAJUMBE wa Baraza la Wawakiishi wameiomba serikali kuweka mikakati itakayohakikisha inawabana maofisa utumishi wa wizara ambao wameanzisha mfumo wa kuiibia serikali kwa kutumia mishahara hewa ya watumishi.

Wajumbe hao walisema baadhi ya maofisa utumishi katika wizara za serikali, wamekuwa wakichakachua mishahara ya watumishi hali inayowafanya wapate fedha nyingi wakati wa kustaafu na hatimaye kuzidokoa fedha za watumishi hao.

Akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija alisema maofisa hao wamebuni mtandao huo ambao ni wa kuiibia serikali.

Mwakilishi huyo alisema anayo orodha za watumishi wa serikali ambao wamekuwa wakilipwa fedha kinyume na kiwango cha elimu walichonacho na kutilia wasiwasi huenda kukawa na mchezo mchafu unaochezewa serikali na maofisa hao.

Akitoa mfano Mwakilishi huyo alisema katika Idara ya Miundombinu sehemu ya utumishi, wapo maofisa wenye kuiibia serikali baada ya kuandaa malipo hewa ambayo hayapo kihalali na yanaonekana kuiibia serikali kwa makusudi.

Alisema kuna watumishi ambao wameandaa malipo yasiyo halali ambapo mfanyakazi mwenye kiwango cha elimu ya cheti amekuwa akilipwa mshahara wa shilingi 399,000 badala ya shilingi 199,000.

Alisema jambo la kusikitisha wafanyakazi hao wapo wengi ndani ya Idara hiyo, ambapo karibuni waliombewa fedha za kiinua mgongo milioni 161, lakini watu hao walichopatiwa ni shilingi milioni 80.

Alisema wafanyakazi hao inadaiwa wamekuwa wakielewana na maofisa utumishi katika wizara za serikali, jambo ambalo linaihujumu serikali kwa kufanya matumizi mabaya yasiozingatia sheria za fedha.

Alisema mambo ya kusikitisha kuona hata baada ya Katibu Mkuu kubaini kuwapo kwa wizi huo uliofanyika na kutaka kuchukuliwa hatua, lakini hadi sasa wahusika hakuna walichofanywa na wanaendelea na utumishi wao.

Kwa upande Mwakilishi wa Jimbo la Wete, Asaa Othman Said, akitoa mchango wake alimtahadharisha waziri kuwa makini na wamiliki wa vyombo vya usafiri baharini kwani wanaonekana ni wenye kupenda kutoa rushwa.

Alifahamisha kuwa imekuwa kawaida kwa baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri baharini kuleta vyombo visivyo na viwango jambo ambalo limekuwa likisababisha watu kupoteza maisha yao kutokana na ajali za baharini.

“Mheshimiwa waziri tumeshachoka kulia na vifo vya baharini na usipojiangalia utajikuta pabaya nakuomba ujiangalie maana hawa watu wanaleta vitu havina kiwango”alisema Mwakilishi huyo.

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza ameishauri serikali kuliangalia suala la matumizi ya V.I.P ya Uwanja wa ndege wa Zanzibar, kwani hivi sasa imeonekana baadhi ya mabalozi kukosa haki ya kutumia sehemu hiyo na kutozwa malipo.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub, alieleza ipo haja ya kuwepo kifaa cha kuongozea meli ili kuweza kusaidia kupunguza maafa baharini huku serikali ikafikiria kulifanyia matengenezo eneo la tawa ya Zanzibar kutokana jumba hilo kuvuja.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, akichangia bajeti hiyo aliiomba uongozi wa wizara hiyo kuyaangalia mafungu mbali mbali likiwemo la safari, kamati, mafunzo, viburudishaji na mafriji.

Mwakilishi huyo pia aliwataka watafiti waliopewa jukumu la kusimamia wizara za serikali kuwa na mbinu mpya za kuiwezesha serikali kufaidika na tafiti zao badala ya kuwapo watu ambao wanaonekana kutokuwa na mafanikio ya aina yoyote katika bajeti zilizoandaliwa.

Nae Mwakilishi wa Kitope Makame Mshimba Mbarouk, akitoa mchango wake juu ya bajeti hiyo alisema yuko tayari kuzuiya kifungu cha mipango na sera kwa Wizara husika kushindwa kulipa fidia ya vipando vya wananchi katika maeneo ya Kilombero.

Alisema kuunduwe tume kumchunguza Mkurugenzi wa Mamlaka usafiri Baharini kutokana na kuipunguzia abiria meli ya Mv. Serengeti kwa kuilazimisha kupakia abiria 300 huku kukiwa na chombo ambacho kimeruhusiwa kupakia abiria 700.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.