Habari za Punde

Masheikh wahimizwa kuelimisha, kushiriki sensa


Na Salama Njani, PEMBA
MUFTI wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, amewahimiza waislamu kufuata mwenendo, mafundisho na sheria za dini ya kiislamu katika kutekeleza mambo muhimu yenye maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Sheikh Kabi alieleza hayo huko mkoa wa Kusini Pemba wakati akiwahutubia Masheikh wa mkoa huo katika semina ya uhamasishaji wa zoezi la sensa ya watu na makazi katika ukumbi wa maabara ya Jamii iliyopo Wawi.

Alisema kufuata maelekezo ya dini pamoja na maagizo ya viongozi wa nchi ambayo hayaharibu na kuvunja amri ya Mwenyezi Mungu, ni njia pekee ya kushiriki na kufanikiwa katika masuala muhimu ya kitaifa.

Alisema serikali inaujua umuhimu wa Masheikh katika nchi ndio maana imekua ikiwashirikisha katika masuala mbali mbali kwa kutoa elimu kutokana na kuwa na kundi kubwa la waumini linalowaamini.

Akitoa mada kuhusu umuhimu wa sensa kwa viongozi hao wa dini Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alisema zoezi la sensa pamoja na kujua idadi ya watu wake, lakini pia inalenga kupanga na kusambaza huduma muhimu za kiuchumi za kijamii kwa kuzingatia kiwango na umuhimu wa mahitaji.

Alisema waislamu wanahitaji kujua idadi yao na takwimu zinazowahusu kiuchumi na kijamii zitakazopeleka mbele juhudi za maendeleo.

Wakichangia mjadala huo washiriki wa semina hiyo walisema viongozi wote wa dini nchini wanawajibu wa kuhamasisha waumini nchi nzima kushiriki zoezi hilo kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

Aidha washiriki hao wameiomba serikali kuwa makini sambamba na kuwachukulia hatua watu au kikudi kinacho husika na utoaji wa takwimu zisizo sahihi ambazo kwa njia moja au nyengine husababisha migogoro kwa jamii.

Akihitimisha semina hiyo Katibu Mufti Sheikh Fadhil Soraga aliwasisitia viongozi hao kuwa pamoja na changamoto zilizopo bado wanawajibu wa kuwaelimisha na kuwahamasisha waumini wao kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo

Semina hiyo yenye lengo la kutoa elimu ya uhamasishaji wa zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 26 i hadi Septemba 1, imewashirikisha Masheikh wa mkoa wa Kusini Pemba pamoja na wawakilishi wa jumuiya za kiislamu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.