Na Mwantanga Ame
WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Nassor Ahmed Mazrui amesema azma ya kulifunga shirika la Magari itatekelezwa, baada ya kufutika kwa malengo yaliyosukuma kuundwa kwa shirika hilo.
Waziri huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali kabla ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara yake.
Mazrui alisema shirika la Magari litavunjwa muda wowote kuanzia sasa kwani limeshindwa kuhimili ushindani na kwamba malengo yaliyopelekea kuunda kwa shirika hilo kuondoka.
Alisema serikali imeamua kuchukua hatua ya kulivunja shirika hilo baada ya kuridhika kushindwa kuleta tija kwa taifa na limekuwa likijiendesha kwa hasara.
Alisema kilichochelewesha kuvunjwa kwa shirika hilo, ni baada ya kujitokeza mambo mbali likiwemo suala la haki na maslahi ya wafanyakazi shirika hilo baada ya kuvunjwa.
Akizungumzia juu magendo ya chakula, alisema serikali haitaruhusu kuendelea kwa vitendo hivyo kwani ni sawa na kuwanyima haki wananchi wa Zanzibar kukosa chakula cha kutosha.
Alisema serikali inahitaji kuendeleza biashara lakini sio kwa mtindo wa magendo ila kinachohitajika ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata sheria za kuingiza vyakula nchini na namna ya kuvitoa bila ya kuwepo udanganyifu.
Aidha, waziri huyo akijibu hoja ya ya suala la maghala ya serikali yaliopo Mtoni kama yaliuzwa kwa mtu binafsi, alifahamisha kuwa wakati akikabidhiwa wizara hakupewa majengo hayo kama ni mali ya wizara hiyo na asingepanda kufukua makaburi ya matendo ya viongozi waliopita kabla ya utawala wake.
Hata hivyo majibu hayo yalimfanya Mwakilishi wa jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija, ashindwe kukubaliana nayo na kudai kuwa kama ni mali ya serikali iliyo chini ya wizara hiyo, ilitakiwa kuwa ndani ya mikono ya wizara hiyo.
Akisaidia jibu la hoja hiyo, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alisema maghala hayo hayajulikani yapo mikononi mwa nani na wizara itahakakikisha inalitambua hilo baada ya kumalizika kwa zoezi la uhakiki.
Akizungumzia suala la ukuzaji viwanda alisema suala hilo linaweza kuwa ndoto kutimizwa kwake kutokana na kuhitajika kuwepo miundombinu mikubwa hasa katika suala la kuwa na bandari ya kisasa.
Alisema pindipo wizara ya Miundombinu na Mawasiliano itaweza kujipanga vizuri na kufanya kazi vya kutosha kubadili sekta hiyo kwa kiasi kikubwa itawezesha kukuza biashara hapa Zanzibar.
Akizungumzia suala la gari za wafanyabiashara wa Zanzibar, kuzuiliwa Tanzania bara, alisema wizara hiyo imeshakutana na wafanyabiashara hao na kuwataka wawasilishe vielelezo juu ya madai hayo, lakini hakuna mfanyabiashara hata mmoja aliyefanya hivyo.
Aidha Mazrui alisema suala la biashara alisema bado hali sio nzuri katika mfumo wa sasa kati ya biashara zinazoenda Tanzania bara kutokana na kuendelea kwa tatizo la utozwaji wa kodi mara mbili.
Alisema tatizo hilo licha ya kufanyiwa kazi kwa muda mrefu lakini bado hali sio nzuri na ni vyema kwa wananchi wakaendelea kulitolea maoni katika Tume ya kutoa maoni ya kuanzishwa mabadiliko ya katiba ya nchi.
Alisema wizara inakusudia kufungua mfuko maalum kwa ajili ya kuinua wafanyabiashara utaokuwa ukifahamika kama RAZA FUND, ambaye wakati wa kuchangia aliahidi kutoa fedha hizo kwa mkopo nafuu usio na riba.
Kuhusu madai ya baadhi ya wafanyakazi kudaiwa kuuza karafuu nje ya nchi badala ya kufanya kazi ya kutafuta masoko waliyotakiwa kuifanya, waziri huyo alisema watendaji hao walifanya hivyo kwa makosa na ni bahati mbaya.
Hata hivyo katika kulishughulikia suala hilo hivi sasa wizara inahitaji kupata muda kuona namna ya kulifanyia kazi suala hilo kwa kuangalia hatua za kinidhamu zitazoweza kuwachukulia watendaji waliohusika na hilo.
Wajumbe hao baada ya mjadala hao wamekubali kuiidhinishia wizara hiyo jumla ya shilingi 5,580 milioni kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
No comments:
Post a Comment