Na Joyce Kassiki, DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalum Riziki Omar Juma (CUF), ameiomba serikali kutoa matibabu na dawa bure kwa wagonjwa wanaokabiliwa na maradhi ya saratani.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati akiuliza suali Bungeni na kusema kuwa ni vyema serikali ikafanya hivyo kutokana na huduma za ugonjwa huo kuwa na gharama kubwa.
Alisema pamoja na tatizo la ugonjwa huo kuwa ni tishio kwa watanzania na dunia nzima, lakini bado matibabu yake hutolewa kwa gharama kubwa.
“Je serikali ina mpango gani wa kutoa bure kabisa matibabu na dawa za ugonjwa huo hasa ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya watanzania bado ni masikini”, alihoji Riziki.
Akijibu suali hilo naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk.Seif Rashid alisema kuwa sera ya nchi imeainisha kuwa huduma za uchunguzi na tiba aina zote za saratani kwa wagonjwa hutolewa bure.
“Tiba hizo ni pamoja na upasuaji, mionzi, dawa za kemikali na vichocheo, zimekuwa zikitolewa bure katika taasisi ya saratani ya Ocean Road, hospitali ya Rufaa Bugando na Rufaa za nje ya nchi mfano India”, alisema Dk.Rashid.
Naibu huyo alifahamisha kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali, dawa zinazonunuliwa zimekuwa hazitoshi kukidhi mahitaji ya wagonjwa wa saratani hivyo kuwalazimu wengine kununua dawa pale zinapokosekana hopsitalini ambapo dawa hizo ni ghali.
Alisema gharama hizo zinafikia hadi shilingi 300,000 kwa sindano moja kwa ajili ya kutibu saratani ya utumbo mpana ambapo tiba yake inahitaji sindano 12 na kufanya jumla ya shilingi milioni 3.6 kiasi ambacho alisema ni kikubwa.
No comments:
Post a Comment