Habari za Punde

Mgogoro CANA umalizwe kunusuru netiboli Afrika

Na Salum Vuai, Maelezo
WAKATI umefika kwa Shirikisho la Vyama vya Netiboli barani Afrika (CANA), kumaliza mivutano inayochangia mchezo huo kushindwa kusonga mbele na kuwakosesha wanaoupenda burudani wanayoitarajia.

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mashirikisho ya Michezo barani Afrika (AASC) Mitchel Tchoya, aliyealikwa kama mwangalizi katika mkutano mkuu wa sekretarieti ya CANA uliofanyika hapa Zanzibar Julai 28 na 29, mwaka huu katika hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Mkutano huo umefanyika ili kutathmini utekelezaji wa majukumu ya CANA mwaka uliopita, matumizi, pamoja na kupanga programu za kutekeleza mambo mbalimbali kipindi kijacho, sambamba na kusaka muarubaini wa kuzika mgawanyiko unaokitafuna chama hicho.

Tchoya alisema, kwa kipindi kirefu sasa, mchezo wa netiboli katika bara hilo, umekumbwa na mgawanyo, mitafaruku ya uongozi na kuingiliwa kwa shughuli zake, ambako kumeongeza ukubwa wa matatizo badala ya kuyapatia ufumbuzi.

Hata hivyo, alieleza kuwa jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Baraza la Vyama vya Michezo Afrika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la uongozi ambalo bado lipo, na kwa bahati mbaya, linaendelea kudidimiza maendeleo ya netiboli barani humu.

“Mwezi Septemba 2011, AASC ilipokea ombi la uanachama kutoka kwa bodi mpya iliyoanzishwa na sehemu ya watu waliojigawa kutoka CANA na ambayo ilitambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Netiboli (IFNA)”, alisema Tchoya.

Kutokana na hali hiyo, na ukweli kwamba AASC inatambua mwanachama mmoja tu, CANA tangu ilipoundwa mwaka 1998, iilishauri CANA ifanye haraka kumaliza tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo, ili mgogoro wa kiuongozi ubaki kuwa historia kwa manufaa ya nchi wanachama na netiboli kwa jumla.

Akizungumza katika ufumbuzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa CANA Sharifa Khamis Salim, alisema ni masikitiko makubwa, kuwa hadi sasa baadhi ya nchi wanachama zimeendeleza msuguano, na kushauri kuwa meza ni sehemu nzuri ya kuyapatia suluhu matatizo yao, ili mchezo wa netiboli uweze kupiga hatua.

Mapema, akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis, alisema ni matumaini yake kuwa, busara na nia njema, kwa wanachama, zitasaidia kuiondoshea CANA mitafaruku na kufungua ukurasa mpya, ili kizazi cha wachezaji wanaoinukia, kipate nguzo imara ya kuwaendeleza katika mchezo wa netiboli.

Mkutano huo uliojumuisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Ghana, Tanzania na nyengine, na kuongozwa na Rais wa CANA, Bi. Carol Garoes, ulifungwa jana kwa kutoka na maazimio kadhaa yanayolenga kuleta ufanisi wa chama hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.