Joseph Ngilisho, ARUSHA
MKAZI mmoja wa Tanganyika pekazi, Moshono jijini Arusha aliyetambulika kwa jina la Andrea Ndokoi anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 65 hadi 70, ameuawa kinyama kwa kuchinjwa shingoni kama kuku na watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, marehemu aliuawa usiku wa kuamkia jana majira ya saa 2:30 usiku kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali wakati akirudi nyumbani kwake, kisha mwili wake kutupwa pembeni ya nyumba yake.
Akizungumzia tukio hilo kaimu kamanda wa polisi mkoani hapa, Zuberi Mombeji alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa marehemu aliuawa wakati akitoka kazini kwake, ambapo hufanyakazi kazi ya ulinzi wa ghala la mbao eneo la Njiro na ni mkazi wa Moshono jijini Arusha.
Mombeji alifafanua kuwa jeshi la polisi lilipata taarifa kutoka kwa mtoto wa marehemu aitwaye, Obadia Andrea (27) ambaye alidai kuwa wakati akirejea nyumbani alikutana na watu kadhaa ambao walimweleza kuwa marehemu baba yake alikuwa ameuawa eneo hilo.
Kufuatia tukio hilo polisi imenzisha uchunguzi wa tukio hilo kwani hadi sasa chanzo halisi hakijajulikana na hakuna mtu yoyote anayeshikiliwa juu ya tukio hilo na mwili wa merehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.
Katika tukio jingine mtu mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka 28 na 30,anayedhaniwa kuwa jambazi ambaye jina lake halikufahamika mara moja aliuawa kwa kupigwa risasi katika majibizano ya risasi na polisi baada ya kukataa kutii amri halali ya polisi waliomzingira nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani hapa, Libaratus Sabas jambazi huyo alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi, wakati akipelekwa katika hospitali ya mkoa Mount Meru kwa matibabu.
Aidha kamanda Sabas aliongeza kuwa polisi ilifanya upekuzi nyumbani kwa jambazi huyo na kufanikiwa kupata bunduki moja aina ya Rifle 458 yenye namba 7052602464 model zkk-620 ambayo alikuwa imekatwa mtutu na kitako ikiwa na risasi 2.
Alisema kuwa askari polisi walikwenda nyumbani kwa jambazi huyo na kuizingira nyumba yake baada ya kuwepo taarifa za uhalifu zinazofanywa na marehemu huyo.
Jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi wa watu wengine wanaoshiriki vitendo vya uhalifu waliokuwa wakishirikiana na marehemu huyo ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.
No comments:
Post a Comment