MWAKILISHI wa kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ‘UN’ Balozi Tuvako Manongi ameeleza kuwa moja kati ya majukumu ya uwakilishi wake kwa nafasi hiyo ni kuiwakilisha na kuyalinda maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yakiwemo na yale ya Zanzibar katika shughuli za Umoja huo.
Balozi Manongi aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ikiwa ni pamoja na kujitambulisha na kumuuaga rasmi Rais.
Balozi Tuvako Manongi alieteuliwa kushika nafasi ya kuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa akiambatana na Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Mwinyi Muombwa.
Katika maelezo yake Balozi huyo alieleza kuwa madhumuni ya mazungumzo hayo ni kuja kusalimia , kujitambulisha na kuaga kufuatia uteuzi wao uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete mwezi wa Octoba mwaka jana na kuwaapisha rasmi mnamo mwezi Juni mwaka huu .
Balozi Manongi alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kukubali ombi lao la kuonana nao kwa madhumuni ya ujio wao huo.
Mwakilishi huyo, aliahidi kufanya kazi kwa uadilifu kwa maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na atatumia maarifa yake yote kuiwakilisha Tanzania kwa kushirikiana na viongozi wenziwe wa ndani na nje.
Balozi huyo alieleza furaha yake kwa kupata nafasi hiyo yenye heshima kubwa ya kuteuliwa kuwa Mwakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa ataienzi heshima hiyo kwa kufanya kazi itakayoendelea kuipa sifa Tanzania.
Nae Dk. Shein alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwateua viongozi hao kushika nafasi hizo. Aidha, Dk. Shein aliwapongeza viongozi hao kwa kukubali uteuzi wao huo na kueleza imani yake kuwa watafanya kazi kwa ufanisi na kutekeleza dhamana walizopewa kwa ari, nguvu na kasi kubwa.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa kazi kubwa tayari imeshafanywa na viongozi waliotangulia kabla yao na imekuwa jambo zuri na la busara kuwa wao wataendelea pale walipofikia wenzao.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao kujitahidi kutilia mkazo yale yote yanayohusiana na maslahi ya Zanzibar na Tanzania nzima kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa yale yanayofanya kazi zake Tanzania pamoja na nchi za nje.
Pia, aliwaeleza viongozi hao kuwa tayari Tanzania imejijengea sifa kubwa katika kutekeleza matakwa ya Umoja wa Mataifa ikiwemo kutekeleza “ONEUN” ambapo hatua hiyo imeweza kufikiwa kwa upande wa Zanzibar na kuwezesha Umoja huo kupitia mashirika yake yaliopo nchini kufanya kazi kwa ufanisi katika jengo moja na kuweza kurahisha utekelezaji wa majukumu ya Umoja huo.
Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya muungano ya Tanzania imepata mafanikio makubwa pamoja na misaada mbali mbali ya kitaalamu kupitia sekta za mbali mbali za maendeleo na ustawi wa jamii kama vile afya, elimu , kilimo, ajira , mawasiliano na nyenginezo.
Alisema kuwa Umoja wa Mataifa umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mipango ya maendeleo ikiwemo MKUZA kwa Zanzibar na MKUKUTA kwa Tanzania Bara pamoja na mipango mbali mbali ya Kimataifa ambapo katika nchi zinazoendelea Tanzania imeweza kufanya vizuri sana na kupata maendeleo makubwa kupitia Umoja huo.
Hata hivyo, mbali ya mafanikio hayo yakiyopatikana, Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa bado kumekuwa na changamoto kadhaa likiwemo suala zima la kukabiliana na maafa hasa yale yanayotokea baharini hali ambayo inatokana na ukosefu wa vifaa, elimu na fedha za kuendeshea kazi.
Dk. Shein alisisitiza kuwa ipo haja kwa viongozi hao mbali na majukumu yao walionapewa pia, wanaweza kuzitumia vizuri fursa za misaada ya kukabiliana na maafa pale zinapotokea ndani ya Umoja huo kwa kutambua kuwa Tanzania pia, ni muhitaji wa misaada ya aina hiyo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao wanaokwenda New – York kushirikiana na viongozi wenzao waliopo Washington DC na viongozi wengine wote huku akiwatakia safari njema na kila la kheir katika kazi zao.
No comments:
Post a Comment