Habari za Punde

Maalim Seif akabidhi Vespa kwa makatibu wa CUF


Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wafuasi wa Chama hicho katika tawi la CUF Kilimahewa mjini Zanzibar, baada ya kukabidhi vespa tisa kwa ajili ya makatibu wa majimbo kwa chama hicho.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akijitayarisha kukabidhi vespa kwa makatibu wa CUF kwa majimbo tisa ya Wilaya ya Magharibi Unguja. Kushoto ni mwakilishi wa viti maalum kupitia chama hicho Mhe. Zahra Ali Hamad ambaye ndiye aliyetoa vespa hizo.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi vespa kwa mmoja wa makatibu wa CUF kwa majimbo tisa ya Wilaya ya Magharibi Unguja.

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa chama hicho na makatibu wa CUF wa majimbo tisa ambao wamekabidhiwa vespa kwa ajili ya kukiimarisha chama. (Picha, Salmin Said, OMKR). 

Hassan Hamad OMKR

 Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, leo amekabidhi vespa tisa kwa makatibu wa CUF kwa majimbo tisa yaliyomo katika Wilaya ya Magharibi Unguja. 

Vespa hizo zenye thamani ya shilingi milioni ishirini na saba zimetolewa na Mwakilishi wa viti maalum kupitia Chama hicho Mhe. Zahra Ali Hamad. 

Akizungumza baada ya kukabidhi vespa hizo, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewataka makatibu hao kuzitumia vespa hizo kwa lengo la kukiimarisha chama na sio kwa shughuli zao binafsi. 


Amempongeza Mhe. Zahra ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali kutokana na moyo wake wa kukitumikia chama, na kuwataka viongozi wa majimbo kuiga mfano wa mwakilishi huyo wa kuteuliwa. 

Majimbo yatakayonufaika na msaada huo ni Dole, Magogoni, Fuoni, Mfenesini, Mwanakwerekwe, Mtoni, Dimani, Kiembesamaki na Bububu. 

Aidha Maalim Seif amewataka Wazanzibari kuimarisha umoja wao na kukataa kurejeshwa walikotoka kwa lengo la kuimarisha ustawi wa jamii na kuharakisha maendeleo ya nchi. 

Makamu wa Kwanza wa Rais ametumia fursa hiyo kuwashajiisha wananchi kushiriki katika sensa ya watu na makaazi, na kufafanua kuwa sensa hiyo ina umuhimu wa kipekee katika pande zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa. 

Kwa upande mwengine Maalim Seif amewahimiza wananchi kushiriki katika kutoa maoni ya katiba kwa uwazi, na kuwasilisha mawazo yao kwa kadri watakavyoona inafaa. 

Amesema Chama hicho kimetoa uhuru wa kutoa maoni kwa wanachama wake, na hakuna mtu atakashinikizwa kutoa maoni asiyoyakubali. “Sisi kwenye Chama chetu hatutishani, kila mmoja ana uhuru wa kutoa maoni yake kwa kadri anavyoona yeye, hatuna tatizo na hilo”, alisema Maalim Seif. 

Nae Mwakilishi huyo ameahidi kuendelea na jitihada zake za kushirikiana na wananchi, na kutoa misaada mbali mbali inayohitajika kwa ajili ya kukijenga na kukiendeleza Chama hicho. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.