Habari za Punde

Shamuhuna Ahimiza Itiqaf Misikiti yote


Na Haji Mtumwa
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, amewashauri waislamu nchini kutumia nafasi ya kumi la mwisho wa Ramadhan kwa kuandaa Itiqaf katika Misikiti yao ili waweze kupata fadhila mbele ya Mola wao.

Shamuhunna aliyasema hayo juzi mara baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano ya kuhifadhi Qur-ann kwa wanafunzi mbali mbali kutoka Zanzibar na nchi za nje huko katika Itiqaf ya Kimataifa inayofanyika Msikiti wa Amani kwa Saidi wa Shoto Wilaya ya Magharib Unguja.

Alisema kuwa ni vyema kwa waislamu nchini kuiga mfano wa uongozi wa msikiti wa Amani kwa Saidi wa Shoto kwa kuandaa Ibada tukufu ya Itiqaf, ili iwawezeshe kujipatia fadhila,hasa katika kipindi kama hiki cha kumalizia mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

"Nawaomba viongozi wa kiislamu wengine kuiga mfano wa msikiti huu katika kuandaa Itiqaf yenye lengo la kutaka fadhila za Mola wao hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadha mwezi ambao ndani yake mna utukufu mkubwa sana" alisema Shamuhuna.

Waziri Shamuhuna aliwanasihi viongozi wa Itiqaf hiyo kuendelea kudumu katika kutayarisha Ibada hiyo ambayo inaonesha umoja na mshikamo kwa waislam kutoka nchi mbali mbali ambao wamefika Zanzibar kuunga na waislam wenzao katika kufanikisha Ibada hiyo ya Itiqaf.

Aidha Waziri huyo aliwanasihi wanafunzi kutovunjia moyo kwa wale ambao hawakubahatika kupata nafasi ya kwanza, akisema kuwa wanafunzi wote wameonesha vipaji vya usomaji ila katika mashindano atakuwapo mshindi wa kwanza na kuendelea.

"Nakupongezeni sana wanafunzi kwa kuonesha uhodari wenu katika kuisoma Qur-ann, ila ni wazi kuwa katika mashindano kutakuwa na mshindi wa kwanza na kuendelea, lakini kwa kweli nyote meonesha vipaji vya hali ya juu katika usomaji wenu.

Mara baada ya nasaha hizo Waziri huyo alikabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo ya kuhifadhi Qur-ann kwa Juzuu moja kwa upande wa wanaume tu, ambapo mshindi wa kwanza alikuwa ni Saidi Omari kutoka Zanzibar aliyepata alama 97 na kujinyakulia televishen ya rangi ya nchi 14.

Huku mshindi wa pili alikuwa ni Abuu Salehe kutoka Pemba aliyepata alama 95, na kujipatia Radio, mshindi wa tatu alikuwa ni mwanafunzi Maneje kutoka Uganda ambaye lizawadiwa Pass ya umeme.

Jamal Ahmed kutoka Kenya alikuwa ni mshindi wa nne kwa kupata alama 58 na kuzawadiwa Dek dvd na mshindi wa tano alikuwa ni Ibrahim Aido kutoka Malawi aliyepata alama 57 ambaye alizawadiwa Set moja ya vikombe.

Naye Waziri Shamuhuna alitoa zawadi kwa upande wake binafsi ambapo mshindi wa kwanza Omar Said kutoka Zanzibar, alimkabidhi mashafu tafsiri ambapo washinhindi waliobakia kila mmoja alikabidhi Juzuu tafsir ya Amma kila mmoja.

Naye Naibu Mwenyekiti wa Itiqaf hiyo Tahir Khatib Tahir, akitoa wito kwa waislam kuunga mkono Itiqaf hiyo kwa kutoa michango yao ili kuiwezesha kufanikiwa vyema.

Alisema kuwa miongoni mwa michango ambayo wanahitaji ni fedha taslim, sukar, Maji pamoja na vyakula vyengine mbali mbali, ambavyo viantumika katika kipindi hiki cha Ramadhan kwa ajili ya kufutarishia.

Itiqaf hiyo inayoanza kila ifikapo mwezi ishirini katika mfungo wa Ramadhani hadi siku ya Idd mosi, imehudhuriwa na wageni mbali mbali wakiwamo kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Malawi, Msumbiji, Tanzania Bara, Zanzibar pamoja na wageni wengine mbali mbali.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.