Masanja Mabula Pemba.
Na Masanja klabu ya soka ya Jamhuri, umesitisha mipango yake ya kutaka kumsajili mchezaji Ibrahim Masaniwa kutoka klabu ya Mundu, kwa madai kuwa mchezaji huyo anapenda anasa na ulevi ndani na nje ya ya uwanja, na hivyo kufanya ashindwe kucheza mpira.
Uchunguzi wa Zanzibar Leo, umebaini kuwa, tayari mchezaji huyo ameshaondolewa kutoka klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Chasasa Wete, na kwamba huduma za kiungo huyo hazihitajiki tena huku kukiwa na mipango ya kutafuta mbadala wake.
Chanzo chetu cha habari kimelieleza gazeti hili, kuwa mchezaji huyo alifukuzwa wakati wa michuano ya Abc Bank Super 8, ambapo timu ya Jamhuri ilitolewa katika hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa mabao 5-1 na Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro.
"Hatuwezi kukumbatia mchezaji mlevi hata awe anacheza kama Messi, kwetu hatakuwa na nafasi, sisi tunawajenga wachezaji kiakili na akiendelea kubakia kwetu anaweza kuwaharibu wachezaji wengine", kilisema chanzo chetu cha habari.
Hata hivyo, Kocha Mkuu wa timu hiyo Ameir Chuwa hakuwa tayari kuthibitisha madai hayo ya kusitisha wa nyota huyo kutoka Tanzania Bara.
Akizungumzia ushiriki wa timu hiyo kwenye michuano ya Super 8, Chuwa alisema vijana wake walionesha uwezo mkubwa, lakini saumu ndiyo iliyosababisha watolewe kwa kipigo kizito na wakata miwa wa Mtibwa.
Kwa upande wake, mchezaji huyo amesema hana taarifa kwamba ametemwa kikosini humo, lakini anashangaa kuonna timu imerudi kutoka Dar es Salaam, bila kumpa fomu za usajili na uhamisho.
Hata hivyo, alisema kwa sasa hawezi kuingia kwa undani juu ya suala hilo, akisema anasubiri kukutana na Meneja wa timu hiyo ili kufahamu hatima yake.
No comments:
Post a Comment