KAMPALA, Uganda
UGANDA imethibitisha kuwa mwenyeji wa mashindano ya Chalenji mwaka 2012, yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Tayari Shirikiho la Soka la Uganda (Fufa), limeteua watu kumi kuunda kamati ya maandalizi ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Fufa, Makamu wa Rais wa shirikisho hilo Moses Magogo, anaongoza kamati hiyo akiwa Mwenyekiti, huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fufa, nyota wa zamani wa Uganda Cranes Edgar Watson, akiwa Katibu wake.
Katika taarifa ya Idara ya Mawasiliano ya Fufa, Watson amesema kuwa, wameshawasiliana na sekretarieti ya Cecafa, na kwamba barua rasmi ya uthibitisho huo, tayari imetumwa jijini Nairobi.
“Michuano hiyo ya Chalenji ya Cecafa, ambayo kwa miaka miwili iliyopita ilifanyika Tanzania, sasa inakuja Kampala kuanzia mwishoni mwa Novemba hadi katikati ya Disemba”, ilisema taarifa hiyo.
Mashindano hayo yatafanyika chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL) Ltd, kupitia kinywaji chake cha Tusker.
Mbali na Magogo na Watson, wengine waliomo kwenye kamati hiyo, ni Patrick Ogwel (Makamu Mwenyekiti), Mujib Kasule, Livingstone Kyambadde, Anthony Kimuli, Rogers Mulindwa, Sam Lwere, Rogers Byamukama na Sam Mpiima ambao wanashika nyadifa tafauti ndani ya Fufa.
Katika hatua ya kwanza kutekeleza majukumu yake, kamati hiyo inatarajiwa kukutana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia michezo wa Uganda, Charles Bakabulindi, kujadili ratiba nzima ya kufanikisha ngarambe hizo za takriban wiki tatu.
Mara ya mwisho Uganda kuandaa mashindano hayo, ilikuwa mwaka 2008, ambapo iliifunga Kenya bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika uwanja wa Nelson Mandela mjini Nambole.
Mwaka jana, timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, ilishinda taji hilo jijini Dar es Salaam kwa kuichapa Rwanda mabao 2-1. (Pana ).
No comments:
Post a Comment