Na Mwantanga Ame
MGOMBEA wa Chama cha TADEA, Seif Salum Seif, amechukua fomu kwa ajili ya kuwania kiti cha nafasi ya Uwakilishi katika Jimbo la Bububu Zanzibar.
Mgombea huyo amechukua fomu hiyo, baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kupuliza kipenga kwa ajili ya kuanza kwa harakati za kuweza kupata wagombea wataoweza kuwania kiti cha Jimbo la Bububu Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Mohammed Ali Mtondoo, kufariki dunia, baada ya kupata ugonjwa wa shindikizo la damu, na kusababisha kiti cha Jimbo hilo kuwa wazi kwa nafasi ya Uwakilishi.
Mgombea huyo alichukua fomu hiyo jana asubuhi katika ofisi za Tume ya Uchaguzi, wilaya ya Magharibi Unguja, baada ya kukabidhiwa na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi Unguja.
Mgombea mwengine ambaye alijitokeza kuchukua fomu hizo ni wa Chama cha SAU, Juma Mitu Domo ambaye anatarajiwa kuingia katika kinyanganyiro hicho ili kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza na Zanzibar Leo baada ya mgombea huyo kuchukua fomu, Katibu wa Chama TADEA, Juma Ali Khatib, alisema dhamira ya Chama hicho kusimamisha mgombea ni kwa kuona umuhimu wa Jimbo ilo kuwa chini ya Chama hicho.
Katibu huyo alisema ni vyema kwa wananchi wa Jimbo hilo, kuona umuhimu wa kumuunga mkono mgombea huyo kwa vile atakuwa tayari kuyatumikia makundi yote ya kijamii ndani ya Jimbo hilo.
Alisema katika Jimbo hilo hivi sasa kumekuwa na tatizo la njia za barabara za ndani na shida ya maji na dhamira ya Chama hicho ni kuoa matatizo hayo wanayaondoa.
Alisema kutokana na na katiba ya Zanzibar hivi sasa inatumia mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, mgombea wa Chama chao atakuwa tayari kufuata mfumo huo kulingana na matakwa ya katiba yanavyotaka katika uendeshaji wa serikali hiyo.
Alisema kinachohitajika hivi sasa ni kuona Tume ya uchaguzi inaandaa mazingira yaliobora ya uchaguzi huo ikiwa ni hatua itayoweza kusaidia Zanzibar kupata sifa ya kumudu kundesha chaguzi zake kwa uhuru na haki.
Aidha, Katibu huyo aliviomba vyama vinavyotarajia kushiriki katika uchaguzi huo navyo kuona vinaendesha kampeni za kistaarabu bila kuwepo kwa matusi ama vurugu zitazoashiria uvunjifu wa amani.
Wakati Chama hicho, kikiwa katika hatua za Tume ya uchaguzi, majina matatu ya wagombea wa Chama cha Mapinduzi, yanatarajiwa kufikishwa mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM ambacho huenda kifanyika Mjini Dar es Salaam, kuanzia leo.
Majina hayo yatafikishwa mbele ya kikao hicho, baada ya wiki iliyopita kufikishwa mbele ya kikao cha Kamati Maalum ya CCM Zanzibar, ambacho kilipendekeza kuyasogeza mbele majina matatu ya wanaotaka kuwani nafasi hiyo.
Majina yanayotarajiwa kufikishwa katika kikao hicho, ni pamoja, Hussein Ibrahim Makungu (Bhaa), ambaye alishika nafasi ya kwanza katika kura ya maoni, Omar Ibrahim Kilupi, na Fatma Adam.
Upande wa Chama cha CUF, kupitia Baraza Kuu la Chama hicho, tayari limempitisha Issa Khamis, kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo ambapo msemaji wake Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani, akizungumza na Zanzibar Leo, alisema chama chao kitahakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na haki na chama chao kitaibuka na ushindi.
Bimani akielezea juu ya matumaini ya chama hicho alisema ni makubwa kwa vile kinatarajia kufanya vizuri katika uchaguzi huo kutokana na mgombea wao kumtumania kwa kiasi kikubwa kuweza kufanya vizuri.
Nacho Chama cha Wakulima na Wafanyabishara Zanzibar, kupitia Mkurugenzi wa Sera wa AFP, Rashid Yussuf Mchenga, hapo awali akizungumzia msimamo wa Chama hicho juu ya hilo, alisema tayari Chama chao kimeshafanya uteuzi wa Mgombea ataewania nafasi hiyo.
Alisema Chama hicho kimteuwa Mussa Ali Mussa na watahakikisha kuwa atashinda baada ya hivi sasa wameanza maandalizi ya kukamilisha taratibu za Tume ya Uchaguzi zinafuata.
Zoezi la uchukuaji wa fomu na urejeshaji kwa ajili ya uchaguzi huo linatarajiwa kukamilika hadi Agosti 30, mwaka huu na uteuzi wa wagombea utafanyika Agosti 30, mwaka huu, huku kampeni zinatarajiwa kuanza Agosti 31, 2012 hadi Septemba 15, 2012, na uchaguzi utafanyika Septemba 16, 2012.
No comments:
Post a Comment