Habari za Punde

Wananchi watakiwa kupuuza ushawishi wa baadhi ya vikundi - Watakiwa kushiriki sensa ya watu na makaazi

Na Salum Vuai, Maelezo 

 MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, amewataka wananchi wa Zanzibar kupuuza ushawishi wa baadhi ya watu na vikundi, unaowataka wasikubali kuhesabiwa katika sensa ya watu na makaazi inayotarajiwa kuanza Jumapili ijayo. 

 Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Vuga, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, sababu za kidini zinazotumiwa na vikundi na watu hao, hazina msingi kwani hakuna dini inayokataza jamii au nchi kufanya hesabu ya watu wake. 

 Mwinyi ameeleza kuwa, zoezi la sensa si kitu cha ajabu kwa Tanzania, kwani nchi zote duniani zinao utaratibu huo unaofanywa kwa lengo la kufahamu takwimu za raia wao ili kujua namna bora ya kujipangia mambo ya maendeleo na mahitaji ya msingi yanayohitajika katika nchi hizo. 


Aidha alisema, serikali zote mbili za Tanzania na ile ya Zanzibar, hazijaona umuhimu wa kuweka masuala ya kujua dini ya mtu kupitia zoezi hilo, kwani waumini wa dini zote wana mahitaji na haki sawa za kuhudumiwa na serikali zao hizo. 

Amefahamisha kuwa, kama kuna watu wanaodai kwamba dini zinakataza watu kuhesabiwa, watoe ushahidi wa aya za vitabu vinavyofuatwa na dini zao, ili kuwapa hao wanaowashawishi sababu nzito zinazoweza kuingia akilini. “Si vizuri kuwaendea watu na kuwataka wasikubali kuhesabiwa kwa kisingizio cha dini bila ya kuonesha ushahidi kitabu gani, aya na kurasa zilizoandika makatazo hayo”, alieleza Mkuu wa Mkoa. 

Akielezea namna serikali zilivyojipanga kufanikisha sensa hiyo, Mwinyi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, alisema, elimu juu ya zoezi hilo imekuwa ikitolewa kwa makarani, maofisa na wasimamizi wa sensa kote nchini, sambamba na kutumia vyombo vya habari kuwaelimsha wananchi ili wajiweke tayari kuhesabiwa. 

Kwa upande wa mkoa wake wa Mjini Magharibi, amesema kwa kushirikiana na ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali, umeunda kamati ya sensa na makaazi ngazi ya Wilaya na Mkoa. “Kamati hizo pamoja na kamati ya sensa, mkoa, zimetoa elimu kwa makundi mbalimbali zikiwemo jumuiya zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, vyama vya siasa na makundi maalum. Na zimepita katika shehia mbalimbali kuwahamasisha wananchi kushiriki sensa”, alisema Mwinyi. 

Amewaomba viongozi wote wa vyama vya siasa, jumuiya mbalimbali, NG’Os, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini, serikali katika ngazi zote na wananchi kwa jumla, kutoa ushirikiano katika kuelimishana na kuhamasisha umma umuhimu wa kuijitokeza kuhesabiwa. 

Aidha amesisitiza haja ya kushirikiana na makarani wa sensa kwa kutoa taarifa sahihi wakati wa zoezi hilo, huku akiwakumbusha watu ambao hawatakuwepo katika kaya zao wakati makarani wakipita, kuacha taarifa zote muhimu zinazowahusu. Sensa ya watu na makaazi ambayo ni ya tano katika historia ya Tanzania, inatarajiwa kuanza Jumapili ya Agosti 26, mwaka huu na kudumu kwa muda wa wiki moja.

 IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO, ZANZIBAR 23 Agosti, 2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.