Habari za Punde

Waziri apongeza mradi wa uhifadhi wa mazingira wa Visiwa vya Barahindi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji akiwakaribisha wataalamu wa uhifadhi wa mazingira ya nchi za visiwa katika Bahari ya Hindi waliofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kuzungumza nae. (Picha, Salmin Said, OMKR).

Khamis Haji (OMKR).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji ameupongeza mradi wa uhifadhi wa mazingira ya nchi za visiwa katika Bahari ya Hindi kwa uamuzi wake wa kuhamasisha jamii ya Wazanzibari umuhimu wa kuhifadhi na kuyalinda mazingira.

Waziri Fereji aliyasema hayo leo huko ofisini kwake Migombani, wakati  alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka mradi huo, uliofika ofisini hapo kumueleza hatua za maandalizi ya mashindano ya insha na uchoraji katuni yatakayofanyika hapa Zanzibar kwa lengo la kuhamasisha suala la uhifadhi wa mazingira.

Amesema uamuzi wa kuihamasisha na kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kuyalinda mazingira ni sahihi kwa sababu utakuza uelewa na kuchangia maendeleo endelevu kwa jamii husika kuepuka uharibifu wa mazingira, jambo ambalo litasaidia kuziweka nchi hizo katika hali ya usalama.

Waziri Fereji amesema nchi za visiwa zinahitajika kuwa na mikakati na mipango imara ya kuzilinda zisiathiriwe kutokana na uhalisia wake, ambapo hupata madhara makubwa, ikiwemo maafa na athari za kiuchumi kutokana na athari za kimazingira.

Naye, Mtaalamu wa Mawasiliano wa mradi huo, Rasoavindrainy Andry amesema insha hiyo itahusu suala la ukataji miti na itazishirikisha skuli tafauti za Zanzibar, zikiwemo za serikali na za watu binafsi.

Alieleza kuwa pia mradi huo utaanzisha mashindano ya uchoraji wa katuni kwa nia hiyo hiyo ya kuhamasisha jamii umuhimu wa kulinda na kuyahifadhi mazingira katika nchi za visiwa.

Mradi wa uhifadhi wa mazingira ya visiwa katika Bahari ya Hindi unahusisha utekelezaji wa maeneo manne ambayo ni, Uhifadhi wa Matumbawe, Usalama baada ya Majanga, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na kusaidia suala la kukuza maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.