Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa M/magharibi afungua kongamano la Bodi ya Mfuko wa barabara

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzíbar        13/09/2012

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdallah Mwinyi Shaabani amewataka  Wakuu wa Wilaya na Maafisa Tawala kufanya kazi kwa mashirikiano na Bodi ya Mfuko wa Barabara wa Zanzibar ili kuhakikisha Barabara zilizopo katika maeneo yao zinatunzwa vyema na kubakia katika hali yake ya ubora muda wote.

Amesema kuwepo kwa mashirikiano ya kutosha kutawawezesha Wadau wote wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya kazi ipasavyo na kuzifanya barabara za Zanzibar kubakia katika kiwango kizuri kinayokubalika kilimwengu.

Abadallah Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua Kongamano baina ya Bodi ya Mfuko wa Barabara na Wakuu wa Wilaya, Makatibu tawala na Mafisa Tawala lenye lengo la kujadili namna bora ya kutunza Barabara za Zanzibar lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mfuko wa Barabara Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 
Amefahamisha kuwa Mfuko wa Barabara Zanzibar ulianzishwa kisheria mwaka 2001 ukiwa na jukumu la kupokea na kutunza fedha kwa ajili ya utunzaji wa Barabara hivyo Kongamano hilo ni miongoni mwa mikakati ya utekelezaji huo.

“Kutokana na wajibu wao wa kisheria ndio maana Wadau wa Mfuko huu wametukutanisha leo hapa kujadili namna bora ya kuweza keendelea kuzitunza barabara zetu kwa kushirikiana kwa pamoja ili ziweze kusaidia kasi ya ukuwaji wa kiuchumi nchini” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Aidha amewataka Wakuu wa Wialaya kwa kushirikiana na Masheha wa maeneo husika kuwasiliana na Wakandarasi wakati wa kazi hizo ili kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo yao wanafaidika na ajira na kuondokana na umasikini.

Kwa upande wao Washiriki wa Kongamano hilo wamedai kufurahishwa na Kongamano hilo kwani limewapatia elimu kubwa ya kujua namna ya kubuni miradi ya barabara na kujua njia sahihi za kukabiliana na uharibifu wa Barabara katika maeneo yao.

Aidha wameiomba Bodi ya Mfuko wa Barabara kuendelea kutoa elimu katika kila Wilaya na kuwashirikisha Masheha na Madiwani ambao ndio wahusika wakuu katika ngazi za chini.

Awali akitoa mada katika Kongamano hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Ali Suleman aliowahakikishia washiriki wa Kongamano hilo ushirikiano wa kutosha na kuwaahidi kuwapatia sheria ambazo zinahusu hukumu ya wale wote watakaobainika kuziharibu barabara.

Katika Kongamano hilo la kujadili namna bora ya kuhifadhi barabara Zanzibar mada mbili kuu zilijadiliwa ambapo mada ya kwanza ilihusu Mchango wa Sekta ya Usafiri kwenye uchumi wa Taifa na mada ya pili ilihusu Kero za barabarani.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 13/09/2012

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.