WATU sita
wanaoshukiwa kufanya vurungu katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.
Watu hao wamefikishwa mbele ya Hakimu Mdhamini wa
mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe, Janet Nora Sekihola kujibu mashitaka ya
shambulio la hatari.
Washitakiwa hao ni Mohammed Ali Amour (39) , Juma
Omar Juma (44) wote wakaazi wa Beitras
na Mohammed Yussuf Ali (28) mkaazi wa Kinuni.
Wengine ni Omar Bakar Faki (40), Khamis Ruwekh
Khamis (25) na Khelef Mohammed Juma (18)
ambao wote ni wakaazi wa Mwanyanya Wilaya ya Magharibi Unguja.
Wote hao kwa pamoja wameshtakiwa kwa makosa matatu
tofauti ya shambulio la hatari chini ya kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu
sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.
Mahakama iliambiwa kuwa washtakiwa hao
waliwashambulia watu watatu tofauti katika maeneo mbalimbali ya miili yao na kuwasababishia maumivu makali.
Waliodaiwa kushambuliwa ni Ashura Machano Makame,
aliepigwa kisu cha mkono wa kushoto kwenye kiganja, Salum Khamis Bakar
aliepigwa kisu kwenye kalio la mkono wa kulia na Hassan Haji Pili aliepigwa
magongo kichwani na mgogoni na sehemu nyengine za mwili wake.
Matukio yote hayo yamedaiwa kutokea Kibweni Wilaya
ya Magharibi Unguja majira ya saa 3:45 asubuhi ya Septemba 16 mwaka huu.
Licha ya washitakiwa hao kukana mashitaka hayo
upande wa mashitaka uliongozwa na Mwanasheria wa Serikali Said Mohammed Ahmed
kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ulidai mahakamani hapo kuwa
upelelezi wake bado haujakamilika.
Hivyo uliiomba mahakama kuiharisha kesi hiyo na
kuipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa ambapo Hakimu Janet aliiharisha
hadi Oktoba 1 mwaka huu.
Washitakiwa wametakiwa kusaini dhamana ya shilingi
500,000 za maandishi pamoja na mdhamini mmoja kila mshitakiwa mdhamini ambae
atawasilisha kima kama hicho cha fedha taslim
pia wawe na vitambulisho vinavyotambulika pamoja na barua za Sheha wa Shehia
wanazoishi.
No comments:
Post a Comment