Na John Gagarini, Bagamoyo
RAIS Jakaya Kikwete amesema barabara ni mshipa wa
fahamu wa uchumi wa nchi .
Aliysema hayo jana katika kijiji cha Kiwangwa
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa uzinduzi wa barabara ya Msata-
Bagamoyo yenye thamani ya shilingi bilioni 89.6.
Alisema kutokana na umuhimu huo nchi yoyote ambayo
haina barabara nzuri haiwezi kuwa na uchumi bora kwani hicho ni kichocheo cha
kuboresha huduma za maendeleo kwa wananchi.
"Barabara ni kiungo muhimu katika kuleta
maendeleo ya nchi yoyote ile hivyo kuzinduliwa barabara hii kutasaidia nchi
kujiletea maendeleo na kwa wakazi wa mkoa wa Pwani ni fursa pekee ya kujiletea
maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo," alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa serikali yake imeweka mikakati
mbalimbali kuhakikisha barabara zinajengwa katika kiwango kinachostahili ili
maendeleo yaweze kukua.
"Wakazi inapopita barabara hii ni vyema
mkatumia fursa iliyopo kujiletea maendeleo yao kwani magari yote kutoka mikoa
ya Kasakazini yatakuwa yakipita hapa hivyo itakuwa ni nafasi yenu kuzalisha
mazao ya chakula na matunda kwa kutumia soko litakalokuwepo," alisema.
Aliwataka wananchi watakaotumia barabara hiyo
kuitunza kwani serikali imetumia gharama kubwa kuijenga hasa ikizingatiwa fedha
hizo ni za ndani na si za wafadhili.
Awali akimkaribisha kuzindua barabara hiyo, Waziri
wa Ujenzi Dk. John Magufuli alisema barabara hiyo ina urefu wa kilomita 64 ambapo
jumla ya kilometa zaidi ya 20 ndizo zilizobakia na inatarajiwa kukamilika
ifikapo Juni 2013.
Dk. Magufuli alisema barabara za kiwango cha lami
zilizojengwa kwa awamu ya nne ni kilomita 11,154 ambapo nchi ilipokuwa inapata
uhuru ilikuwa ni kilomita 1,330 na baada ya miaka 50 ilikuwa ni kilomita 6,500
za lami.
"Nitashangaa kusikia watu wakisema kuwa
serikali haijafanya lolote tuwe wakweli
haya yaliyofanyika ni maendeleo hivyo lazima tuipongeze serikali yetu
kwa kupiga hatua na tusimsifie mtu anapokufa tumsifu hata kabala hajafa kwani
kama kafanya jambo zuri lazima tumpongeze," alisema Dk. Magufuli.
Alisema anashangaa kusikia watu wakibeza safari za
nje za rais lakini ndizo zilizozaa matunda kama
hayo na kusisitiza kuwa mtu anapoomba
lazima akutane na yule anayemwomba.
Alitoa wito kwa wale wote waliolipwa kupisha
barabara hiyo kuondoka kwenye eneo la hifadhi ya barabara na wale watakaojenga
sasa hawatalipwa fidia yoyote.
Ujenzi wa barabara hiyo ulianza mwaka 2008 ambapo
kampuni ya kwanza ya Tacopa ilinyang’anywa ujenzi huo mwaka mmoja baadaye baada
ya kushindwa kutekeleza makubaliano.
No comments:
Post a Comment