Na Juma Mmanga, Dar
WAJUMBE wa Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na
Habari ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, wameshauri kuongezwa ushirikiano
kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na
Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) ili
kusaidia harakati za maendeleo nchini kwa vile vyombo hivyo ni mali
ya umma.
Wajumbe hao walieleza hayo walipotembelea Ofisi za
TBC 1 na TBC Taifa, katika ziara ya kikazi iliyoandaliwa na Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii ili kuwajengea uelewa Wajumbe hao kuhusiana na uendeshaji wa
vyomb vya habari nchini.
Akitoa shukurani kwa uongozi wa TBC, Mjumbe wa
Kamati hiyo, Asaa Othman Hamad, alisema kuna umuhimu mkubwa wa vyombyo hivyo
kusaidiana kwani malengo yake yanafanana ambayo ni kutoa taaluma na
kuwaelimisha wananchi kushiriki katika mipango ya maendeleo nchini.
Mapema Kamati hiyo ilitembelea Ofisi za Wizara ya
Habari, Utalii na Michezo Zanzibar zilizoko jengo la Wizara ya Fedha Zanzibar
Mjini Dar es Salaam, kuona studio ya ZBC na kuzungumza na wafanyakazi wa ofisi
hiyo.
Mbali ya kupongeza juhudi zinazochukuliwa na
wafanyakazi wa Ofisi hiyo, Kamati hiyo ilipongeza hatua ya Wizara kuanzisha
ofisi Dar es Salaam, ambayo itasaidia kuimarisha ushirikiano pamoja na
kuchangia kuongezeka mapato ya Serikali.
Jioni Kamati hiyo ikifuatana na Uongozi wa Wizara
ya Habari, chini ya Naibu Waziri wake Bihindi Hamad Khamis na Naibu Katibu
Mkuu, Issa Mlingoti, ilitembelea Chuo cha Utalii Dar es Salaam, ili kuona namna
chuo hicho kinavyoendeshwa ili kupata cha kushauri katika uendeshaji wa Chuo cha
Maendeleo ya Utalii Zanzibar.
Kamati hiyo iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wake,
Mohammed Said Dimwa na Wajumbe Ali Mzee Ali, Asaa Othman Hamad, Salim Abdalla
Hamad, Abdi Mosi Kombo, Kazija Khamis Kona, Viwe Khamis Abdalla na Bihindi
Hamad Khamis, ambae pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment